
Video ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalohisika na masuala ya wakimbizi UNHCR iliyotumwa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa inaonesha msururu wa watu wakitembea barabarani, wakubwa kwa watoto, wengine wakiwa wamebeba vifurushi kichwani, wengine wameweka mizigo kadhaa kwenye baiskeli na wengine wakiwa hawana chochote.
Kisha video inaonesha watu wengi mno, wakiwa katika eneo la wazi, wengine wakiwa ndani ya makazi yao ambayo yamejengwa kwa miti na maturubai yenye nembo ya UNHCR, hapa ni Ndava jimboni Bujumbura nchini Burundi na haya ndio makazi ya muda ya wakongomani waliokimbia machafuko nchini mwao.
Mmoja wa wakimbizi hawa ni Sikitu Giginya, akiwa amezungukwa na watoto wengi, anatueleza hali ilivyo hapo.
“Hali ya hapa ni ngumu, chakula hakuna, kutafuta kuni, maji na hata sehemu ya kuogea hakuna. Tunalala kwenye udongo, hakuna nyumba, mvua jana ilitunyeshea, tulilowana na watoto hawana viatu wala kitu cha kula, tuna njaa mpaka wakati huu. Tunaenda tunatafuta na kuomba kuchuma mboga za majani , nilikutana na baba mmoja akanionea huruma akaniambia mama pole, akaniruhusu kuchuma mboga na kuzitwanga kwakutumia kinu chake.”
Maafisa wa UNCHR nao wapo katika eneo hilo wakipita na kuzungumza na wananchi hayo ili kuweza kusikia yale wanayohitaji kwas asa.
Brigitte Mukanga-Eno, ni mwakilishi wa UNHCR nchini Burundi
“Tulianza kupokea wakimbizi kutoka DRC Ijumaa ya Desemba 5. Tangu wakati huo, tayari idadi ya watu imezidi 40,000 katika wiki moja tu. Hii ni kutokana na mapigano makali sana upande wa Congo. Watu walianza kuingilia Kamanyola, na tuliona watu wengi wakivuka kutafuta usalama nchini Burundi. Walitokea Sange, lakini pia kutoka Katogota. Kama unavyoona, kuna watoto wengi, wazee, wagonjwa, na watu ambao wamejeruhiwa na kila kitu kilichotokea Congo. Kwa hivyo UNHCR na Umoja wa Mataifa nchini Burundi kwaujumla tunajaribu kupanga usaidizi wa muda huu. Huu ni mwanzo tu, idadi kubwa ya watu wameendelea kuwasili katika siku za hivi karibuni.”
UNHCR nchini Burundi inafanya kazi kwa karibu na serikali ya nchi hiyo pamoja na washirika wengine ili kuongeza haraka ulinzi, na uwezo wake wa uendeshaji ili kushughulikia mahitaji ya dharura ya wakimbizi wapya wanaowasili ikiwa ni pamoja na usaidizi wa kuokoa maisha, kupanua vituo vya mapokezi na ufuatiliaji wa ulinzi na huduma muhimu.