
Akizungumza na vyombo vya habari hii leo kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York baada ya kutoa taarifa kwa Baraza la Usalama, Katibu Mkuu Antonio Guterres amesema mvutano “unaendelea kutokota kote Yemen,” huku hatua za hivi karibuni za vikosi vinavyohusishwa na Baraza la Mpito la Kusini STC katika maeneo ya Hadramawt na al-Mahra vikizua wasiwasi mkubwa.
“Hatua za upande mmoja hazitafungua njia ya amani,” amesema Katibu Mkuu, “Zinazidisha migawanyiko, zinakaza misimamo, na kuongeza hatari ya kuongezeka kwa mapigano na kusambaratika zaidi.”
Hatari ya athari za Kikanda
Katibu Mkuu ameonya kuwa kurejea kikamilifu kwa mapigano nchini Yemen kunaweza kuwa na athari kubwa kwa amani na usalama wa kikanda, ikiwemo kwenye njia muhimu za baharini.
Ameonya kuwa “Kurejea kikamilifu kwa mapigano kunaweza kuwa na madhara makubwa kwa amani na usalama wa kikanda ikiwemo katika Bahari ya Shamu, Ghuba ya Aden, na Pembe ya Afrika”.
Amewataka wahusika wote wa Yemen na wadau wa kikanda kujizuia kwa kiasi kikubwa na kuunga mkono juhudi za upatanishi zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa.
“Uhuru na umoja wa ardhi ya Yemen lazima vilindwe,”amesisitiza.
Wito wa suluhu ya kisiasa iliyojadiliwa
Akirejea msimamo wa muda mrefu wa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu amesema Yemen inahitaji kwa dharura suluhu ya kisiasa ya kudumu inayopatikana kupitia mazungumzo, si kwa nguvu.
“Yemen inahitaji suluhu ya kisiasa ya kudumu, iliyojadiliwa inayokumbatia matarajio ya Wayemen wote na kumaliza mgogoro huu wa uharibifu,” amesema.
Amebainisha kuwa ingawa amani iliwahi kuonekana kuwa karibu, ikiwemo kipindi cha usitishaji vita cha mwaka 2022 na ahadi zilizokubaliwa mwaka 2023, maendeleo ya hivi karibuni yamezorotesha hali hiyo.
Janga la kibinadamu linaongezeka
Katibu Mkuu amesisitiza gharama kubwa ambayo raia wanaendelea kulipa, akielezea hali ya kibinadamu kuwa mbaya sana.
Takribani watu milioni 4.8 wamekimbia makazi yao, na watu milioni 19.5 wanahitaji msaada wa kibinadamu, amesema.
Ameongeza kuwa “Hadi pale amani itakapopatikana, wananchi wa Yemen wataendelea kulipa gharama kubwa mno.”
Licha ya changamoto za kiutendaji, Umoja wa Mataifa na washirika wake wamewafikia zaidi ya watu milioni 5.3 mwaka huu kwa msaada wa chakula, lishe, maji na huduma za afya.
“Kwa ufadhili wa kutosha na nafasi ya kufanya kazi bila vikwazo, tunaweza kufanya zaidi,” ameongeza Guterres.
Kukamatwa kwa wafanyakazi wa UN
Katibu Mkuu amelaani vikali kuendelea kushikiliwa kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na washirika wao katika maeneo yanayodhibitiwa na Wahouthi, akisema mazingira ya kazi yamekuwa “yasiyovumilika.”
Ameongeza “Ninalaani vikali kuendelea kushikiliwa kiholela kwa wafanyakazi 59 wa Umoja wa Mataifa na washirika,” akitaka waachiliwe mara moja na bila masharti yoyote.
Pia amelaani kupelekwa kwa wafanyakazi watatu wa Umoja wa Mataifa katika mahakama maalum ya jinai, akisema mashitaka hayo lazima yafutwe.
“Wameshtakiwa kwa kutekeleza majukumu yao rasmi ya Umoja wa Mataifa. Mashitaka haya lazima yaondolewe,” amesema.
“Kuendelea kuzuiliwa kwa wenzetu ni dhuluma kubwa kwa wale wote wanaotumia maisha yao kuwahudumia wananchi wa Yemen.”
Amani bado inawezekana
Licha ya kuongezeka kwa mvutano, Katibu Mkuu aamesema bado kuna njia ya kufikia amani, akiwataka wahusika wote kushirikiana kwa dhati na Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa.
“Hata hivyo, njia ya amani bado ipo,” amesema. “Umoja wa Mataifa unabaki kujitoa kikamilifu katika kuwaunga mkono wananchi wa Yemen kwenye safari hii.”
Alihitimisha kwa wito mzito kwa pande zote “Wananchi wa Yemen wanadai na wanastahili amani.”