Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amesema idadi ya wahamiaji wanaokimbia machafuko katika mji wa Uvira, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imeongezeka na kufikia watu 202.

Kauli hiyo inakuja siku moja baada ya ripoti kuonesha waasi wa M23, waliokuwa wakipambana na Jeshi la DRC, wameachia mji wa Uvira.

Hata hivyo, idadi ya raia wanaovuka mpaka na kuingia Tanzania kutafuta hifadhi na usalama imeendelea kuongezeka.

Kwa mujibu wa Balozi Sirro, Desemba 14, 2025, walikamatwa wahamiaji 52, huku jana, Jumanne, Desemba 16, 2025, wakikamatwa wengine 150. Wote walikamatwa wakiwa kwenye vyombo vya usafiri na wakiwa wamechanganyika na raia wa kawaida wa Tanzania.

Akizungumza na Mwananchi leo, Desemba 17, 2025, Balozi Sirro, ambaye pia ni Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) mstaafu, amesema kukamatwa kwa wahamiaji hao ni sehemu ya operesheni zinazoendelea za kulinda ulinzi na usalama mkoani Kigoma.

“Jana tumewakamata wahamiaji wengine 150, na hivyo jumla yao kufikia 202. Wote wanaendelea kuhojiwa na vyombo vya ulinzi na usalama, na taratibu zikikamilika tutawakabidhi UNHCR kwa ajili ya kupelekwa makambini,” amesema.

Amesema uchunguzi huo unalenga kujiridhisha kuhusu usalama wao ili kuhakikisha hawaingizi vitu vinavyoweza kuhatarisha usalama wa nchi.

“Mchakato wa kuwahoji unaendelea. Tukiridhika kuwa hakuna changamoto za kiusalama, watahamishiwa makambini. Hata hivyo, napenda kuwahakikishia wananchi kuwa Mkoa wa Kigoma uko shwari na shughuli za kiuchumi zinaendelea kama kawaida,” ameongeza.

Wakati huohuo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limesema ndani ya wiki moja pekee, watu takriban 30,000 wameingia nchini Burundi, huku Umoja wa Mataifa ukieleza mapema wiki iliyopita kuwa zaidi ya watu 200,000 wameyakimbia makazi yao mashariki mwa DRC.

Uvira ni mji uliopo mashariki mwa DRC na ni moja ya maeneo ya kimkakati yenye bandari na njia rahisi za maji kuelekea Rwanda, Burundi, Tanzania na Zambia, uliangukia mikononi mwa waasi wa M23 Desemba 10, 2025, baada ya Jeshi la DRC kuondoshwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *