TIMU ya Kombaini ya Makamba ya Burundi na Kombaini ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ya mkoa Kigoma, Tanzania zinatarajia kumenyana katika mchezo wa fainali ya mashindano ya ujirani mwema ya timu za mikoa ya Burundi na kombaini za wilaya za mkoa wa Kigoma.

Kombaini ya Makamba ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuingia fainali baada ya kuifunga timu ya mkoa wa Ruyigi katika mchezo wa nusu fainali kwa kufunga goli 2-1 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Nkurunzinza Peace Park Complex wilaya ya Makamba mkoa wa Burunga.

Mkurugenzi wa maendeleo ya michezo wa Wizara ya Michezo, Sanaa na utamaduni, Burundi, Yussuph Singo (wa pili kulia) akikagua timu ya Kombaini ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kabla ya kuanza mchezo wa nusu fainali baina ya timu hiyo na Kombaini Ya Buhigwe zote za Tanzania (Picha na Fadhili Abdallah)

Magoli ya Kombaini ya Makamba yalifungwa na Niyomwungere Claude dakika ya 26 ya mchezo na goli la pili likifungwa na Ntakirutimana Jules dakika ya 40 wakati goli la Ruyigi limefungwa na Fabric Nitunga dakika ya 71.

Kwa upande wake Kombaini ya Manispaa ya Kigoma Ujiji imeingia fainali baada ya kuifunga Kombaini ya wilaya ya Buhigwe kwa magoli 3-2 katika mchezo wa kusisimua ambao ulikuwa na mshindani mkubwa kila timu ikitaka kucheza fainali.

Sehemu ya kikosi cha Kombaini ya Makamba kutoka mkoa Burunga, Burundi (Picha na Fadhili Abdallah)

Magoli ya Manispaa ya Kigoma Ujiji yalifungwa na mshambuliaji wake hatari Maneno Saidi katika dakika ya 27, dakika ya 44 na dakika ya 62 ya mchezo ambapo magoli ya Buhigwe yalifungwa na Zanzari Yekonia dakika ya 36 na dakika ya 55 ya mchezo huo.

Aidha kipindi cha pili Mchezo wa Manispaa ya Kigoma Ujiji Ibrahim Amani alipata kadi nyekundu baada ya kumchezea madhambi mchezaji wa Buhigwe ndani ya eneo la 18 na hivyo Buhigwe kupata penati ambayo hata hivyo mpigaji Imani Gerson alikosa baada ya mpira kugonga mwamba na kurudi uwanjani ukiokolewa na wachezaji wa Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Mkurugenzi wa maendeleo ya michezo wa Wizara ya Michezo, Sanaa na utamaduni ya Burundi, Yussuph Singo (wa pili kushoto) akikagua timu ya Kombaini ya wilaya ya Makamba mkoa Burunga nchini humo. (Picha na Fadhili Abdallah)

Mkuu wa mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro, wakuu wa wilaya, wakurugenzi na viongozi mbalimbali wa mkoa huo anatarajia kuhudhuria mechi hiyo ya Fainali nchini Burundi huku wakuu wa mikoa mbalimbali ya Burundi na viongozi waandamizi wa nchi hiyo wakitarajia kushuhudia pia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *