
Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Hati za Mizigo Zinazoweza Kuhamishika (UN Convention on Negotiable Cargo Documents) unaanzisha, kwa mara ya kwanza, hati moja inayoweza kutumika kwa treni, malori na ndege, na kuruhusu mabadiliko ya kimkakati ya usafirishaji kufanywa kwa bidhaa ambazo tayari ziko safarini.
Hii ina maana kwamba mizigo ya thamani inaweza kuuzwa, kubadilishiwa mwelekeo au kutumika kupata ufadhili wakati wa safari ambayo inaweza kuwa ndefu sio tu kabla ya kupakiwa.
“Hili ni jambo la kubadili mchezo kabisa kwa biashara ya kimataifa,” anasema Anna Joubin-Bret, Katibu wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Sheria ya Biashara ya Kimataifa (UNCITRAL), iliyoongoza mazungumzo ya miaka mitatu. “Hati moja ya usafiri iliyo ya aina nyingi (multimodal), ya kielektroniki kikamilifu, na inayoweza kuhamishika.”
Kutoka Brazil hadi Paraguay, kupitia Azerbaijan
Kwa sasa, hati za usafiri zinazoweza kuhamishika hutumika zaidi kwa bidhaa zinazosafiri kwa bahari, ambako safari zinaweza kuchukua wiki kadhaa. Bidhaa kama mafuta au kakao mara nyingi huuzwa mara kadhaa zikiwa baharini bei zinapobadilika.
Kinyume chake, bidhaa zinazosafiri kwa barabara, reli au anga kwa kawaida hupelekwa kwa mnunuzi mmoja na mahali pamoja hali inayopunguza kubadilika na upatikanaji wa zana za kifedha.
James Hookham, Mkurugenzi wa Global Shippers Forum, alieleza mfano wa kubuni wa mzigo wa bidhaa ukisafiri kutoka kwa muuzaji nchini Brazil kwenda kampuni tanzu nchini Paraguay.
“Hali ya soko hubadilika,” anasema Bwana Hookham. “Bidhaa zikiwa safarini ambayo inaweza kuchukua siku kadhaa unaweza kupata mnunuzi anayekubali kulipa bei nzuri zaidi mahali pengine.”
Chini ya mfumo mpya, anasema, bidhaa hizo zinaweza kuuzwa katikati ya safari kwa mnunuzi, kwa mfano, nchini Azerbaijan, na kubadilisha mwelekeo zikiwa njiani. “Ni kama kufuta anwani kwenye bahasha baada ya tayari kuwa imetumwa kwa posta.”
Bidhaa zilizokuwa zikielekea Paraguay kwa meli zingeweza kuchukuliwa kwa ndege hadi Istanbul, Türkiye, kisha kupelekwa kwa treni hadi Azerbaijan yote hayo yasingewezekana chini ya masharti ya sasa.
Faida pana
Urahisi huu unazidi kuwa muhimu kadiri njia mpya za biashara zinavyofunguliwa kote Asia ya Kati, kati ya China na Ulaya, na barani Afrika mara nyingi zikihusisha njia zinazohudumia nchi zisizo na bandari.
Mkataba mpya “unakuruhusu kutoziacha tu bidhaa kwa sababu tarehe ya mauzo imepita,” anasema, akiongeza kuwa vyanzo vya misukosuko katika biashara ya kimataifa vinaendelea kuongezeka.
Bwana Hookham alitaja athari hasi za misukosuko ya hivi karibuni ya ushuru, matukio yasiyotabirika ya hali mbaya ya hewa kama vile Kimbunga Melissa kilichovuruga njia za biashara katika eneo la Karibe na utekaji wa mizigo katika Bahari ya Shamu.
Mkataba huo unalenga kupunguza hatari kwa benki na wasafirishaji kwa kutoa kanuni za kisheria zilizo wazi kuhusu nani anamiliki mzigo wakati wowote. Uhakika huo wa kisheria, alisema Bwana Hookham, unazifanya benki kuwa tayari zaidi kufadhili mikataba na kuwasaidia wasafirishaji kuepuka migogoro ya kupeleka bidhaa kwa mhusika asiye sahihi.
“Ikiwa Mpango A hautakufaa, au utakugharimu fedha nyingi, huu ndio mbadala,” anasema.
Nani wa kwanza kusaini?
Mkataba huu utakuwa muhimu hasa kwa nchi zisizo na bandari na nchi zinazoendelea, kwa kuwasaidia kujiunganisha zaidi na mfumo wa biashara ya kimataifa na kupunguza gharama.
Tayari kuna hamasa kutoka kwa nchi za Afrika na Asia ya Kati, pamoja na mataifa makubwa ya biashara ikiwemo China, ambayo ilianzisha mchakato ulioleta mafanikio ya wiki hii katika Umoja wa Mataifa mwaka 2019.
Mchakato wa mazungumzo, ulihusisha mashauriano mapana, ni mfano wa “ushirikiano wa kimataifa unaofanya kazi kwa ufanisi,” anasisitiza Bi. Joubin-Bret.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio linalounga mkono mkataba huo tarehe 15 Desemba 2025. Hafla ya kutia saini imepangwa kufanyika nusu ya pili ya mwaka 2026 mjini Accra, Ghana.
Mkataba utaanza kutekelezwa mara tu nchi kumi zitakapouridhia.