Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku hii inayoadhimishwa kila mwaka 18 Desemba amesisitiza kuwa wahamiaji “huchochea uchumi, kuunganisha tamaduni, na kunufaisha nchi za asili na zinazopokea,” akibainisha uwezo wa uhamiaji salama na unaosimamiwa vyema kuleta mabadiliko makubwa.
Timu za IOM zinatoa msaada wa dharura wa matibabu kwa wahamiaji wanaposhuka kwenye bandari ya Abusita huko Tripoli, Libya.
Changamoto na hatari
Licha ya manufaa yake, Guterres amesema uhamiaji unaleta hatari kubwa pale unapoendeshwa vibaya au kutafsiriwa kinyume na ukweli.
Tangu 2014, karibu wahamiaji 70,000 wamekufa au kupotea katika njia za nchi kavu na baharini, huku wanawake na watoto wakiwa miongoni mwa walio hatarini zaidi.
Ameongeza kuwa mipaka inazidi kufungwa, huku wahalifu wa usafirishaji haramu wa binadamu na uharamia wakiendelea hatarisha maisha ya wale wanaotafuta usalama au fursa.
Makubaliano ya kimataifa kuhusu uhamiaji salama
Miaka saba iliyopita, jumuiya ya kimataifa ilipitisha Makubaliano ya Kimataifa kwa Uhamiaji Salama, Unaopangwa na wa Kawaida, kwa lengo la kuongeza faida za uhamiaji huku ikitatua changamoto zake.
Katibu Mkuu amesema, “Tunaweza na lazima kutumia nguvu ya uhamiaji kusongesha maendeleo endelevu na kujenga jamii zilizo imara zaidi.”
Katika MRC, wafanyakazi wa IOM kama vile Kadija wanasaidia watoto wahamiaji na watu wazima katika kujenga uwezo wa kustahimili ustahimilivu kupitia sanaa na uchezaji baada ya uzoefu mgumu.
Uhamiaji kama hadithi ya kibinadamu
Mkurugenzi Mkuu wa Sjhirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM, Amy Pope, katika ujumbe wake amebainisha kipengele cha kibinadamu cha uhamiaji, akisema, “Uhamiaji umegusa maisha ya familia na jamii kila mahali. Ni hadithi ya ujasiri, azimio na uhusiano unaotuunganisha kuvuka mipaka.”
Ameeleza haja ya mshikamano wa kimataifa katika kuunda mifumo ya haki na jumuishi inayowalinda wahamiaji na kusaidia jamii zinazowapokea.
Michango ya kiuchumi na kijamii
Wahamiaji huchangia katika uchumi wa eneo kwa kujaza pengo la ajira muhimu, kuendeleza ujasiriamali, na kutuma mabilioni ya dola kama misaada ya kifedha kwa familia zao nyumbani.
Kwa mujibu wa IOM mwaka 2024, misaada ya kimataifa ya fedha zinazotumwa nyumbani na wahamiaji ilifikia takriban dola bilioni 905, ikisaidia kaya kufidia chakula, elimu, na huduma za afya, mara nyingi zikizidi thamani ya misaada ya kigeni.
Vijana wakishiriki katika WakaWell Hackathon ili kubuni masuluhisho ya kidijitali kwa ajili ya uhamiaji salama na wenye ujuzi.
Kuelekea uhamiaji salama na uliopangwa
IOM imesema ingawa uhamiaji mkubwa hufanyika salama, wengi bado wanakabiliwa na hatari katika safari zao kutokana na upungufu wa njia rasmi.
Umoja wa Mataifa na shirika la IOM wanahimiza nchi kuimarisha mifumo inayowalinda wahamiaji na kuwezesha uhamaji kuwa wa heshima.
Katibu Mkuu amesema, “Safari ya kila mhamiaji ni tofauti, lakini hitaji la usalama na heshima ni la pamoja.”
Katika Siku ya Kimataifa ya Wahamiaji mwaka huu, jamii zinakaribishwa kushiriki hadithi zao za uhamiaji kupitia #MyGreatStory, zikisherehekea uvumilivu na michango ya wahamiaji duniani kote.