Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa amewafanyia mahojiano kwa nyakati tofauti vijana wanne waliowahi kupata fursa ya kujifunza kwa vitendo katika idhaa hiyo na ambao wanaendelea na mafunzo kwa sasa.
Balozi Gertrude Mongella (kulia) kutoka Tanzania, akiwa na Sabrina Moshi wa UN News Kiswahili.
Sabrina Saidi
Yeye ni mhitimu wa shahada ya mawasiliano ya Umma kutoka chuo kikuu cha mtakatifu Augustino, SAUT kilichopo Mwanza nchini Tanzania na kwasasaanashiriki mafunzo kwa vitendo katika idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa akiwa Kitengo cha habari cha Umoja wa Mataifa, UNIC Dar Es Salaam.
Sabrina ambaye anatarajia kuhitimu mafunzo hayo mwanzoni mwa 2026 anasema “kwanza hii ni fursa kubwa sana kwangu kushiriki mafunzo kwa vitendo UN, najifunza kwa vitendo zile nadharia nilizojifunza darasani kama kuandika habari, kuihariri na kuichambua.”
Ameeleza pia anavyoshirikiana na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa “Ninapata uangalizi na usimamizi kutoka kwa waandishi wabobezi wa habari wanaofanyaka katika Umoja wa Mataifa. Uwepo wangu hapa unanipa fursa ya kujifunza Kiswahili (Fasaha).”
Wito wake “kwa vijana ambao wapo vyuoni na ambao bado hawajamaliza chuo nikwamba watafute fursa kama hizi wasiziache, wakumbatie fursa kama hizi za Umoja wa Mataifa wasiziache.”
Ahimidiwe Olotu, Mfanyikazi kwa mafunzo wa Umoja wa Mataifa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.
Ahimidiwe Olotu
Wakati dunia imejifunzia na inapambana na janga la coronavirus“>COVID-19 mwaka 2020- 2021 Ahimidiwe alipata fursa ya kushiriki mafunzo kwa vitendo nchini Tanzania naye akiwa UNIC Dar es salaam nchini Tanzania. Akiwa hapo alifanya kazi pia moja kwa moja na Idhaa ya Kiswahiki kutoja New York Marekani.
“Kwakifupi naweza kusema Umoja wa Mataifa ulichora njia ya mafanikio yangu ya Uandishi wa habari kwasababu nilipata nafasi ya kujifunza vitu vingi hususani katika ufanya kazi ya uandishi wa habari kwani nilikuwa nafanya kazi New York na Dar es Salaam.”
Olotu anasema fursa ya kufanya kazi na wabobezi wa uandishi wa habari ulimjengea uwezo mkubwa kwenye si tu kaundaa bali pia kuwasilisha habari hadi kufikia hatua ya kuwa na ujuzi wa aina mbalimbali katika fani ya uandishi wa habari.
“Mafunzo kwa vitendo ambayo nilifanya katika Umoja wa Mataifa yalinifanikisha kuchora njia pana ya mimi kufikia hapa nilipo. Baada ya kumaliza mafunzo ambapo nilijifunza vitu vingi nilifanikiwa kuondoka sababu nilipata kazi katika moja ya chombo cha utangazaji kikubwa nchini Tanzania – Azam Media ambapo ndipo ninafanya kazi mpaka sasa hivi, na nimeweza kuonesha yale ambayo nilijifunza kutoka Umoja wa Mataifa kwa vitendo.”
Mtangazaji huyu maarufu nchini Tanzania anasema ukipita Umoja wa Mataifa masuala mengi unayaangalia kwa viwango vya kimataifa akitolea mfano utendaji kazi wake, “Katika utendaji kazi wangu nazingatia au kujumuisha Malengo 17 ya Maendeleo endelevu SDGs ambayo ni mtambuka na yanagusa kila sehemu katika uandishi wa habari.”
Kwenye suala la kuchangamkia fursa Ahimidiwe anasema “Ninachowasisitiza vijana ni wanapoona fursa zinazotolewa na Umoja wa Mataifa hususani zinazohusu mafunzo kwa vitendo wasiache kuzichangamkia, wajitokeze, wafanye maombi na huenda wakachaguliwa kama ambavyo mataifa mengine wanafanya mfano Kenya ambapo vijana wake wanachangamkia fursa za aina hii wanapoziona tu .”
Sheilah Jepng’etich
Kwa wale wenye uwezo wa kujifadhiliwe wenyewe kuishi jijini New York Marekani, fursa ipo ya kufanya mafunzo kwa vitendo katika Makao Makuu ambapo mbali na kujifunza yanayoendelea katika idara ya mawasiliano ya umma ya Umoja wa Mataifa pia mshiriki anapata fursa ya kutashuhudia yote yanayoendelea katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mfano Mikutano ya Ngazi za juu na ule maarufu zaidi duniani wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA unaofanyika kila mwaka mwezi Septemba ambao huwaleta pamoja wakuu wa nchi na serikali kujadili masuala mbalimbali na kuweka mustakabali bora wa dunia.
Sheilah Jepng’etich, Mfanyakazi kwa mafunzo wa Umoja wa Mataifa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.
Sheilah Jepng’etich kutoka nchini Kenya amechangamkia fura hiyo na sasa anashiriki mafunzo kwa vitendo jijini New York na anasema “nimeweza kuimarisha sana na kuandika habari lakini kando na hayo nimeweza pia kutangamana na watu kutoka duniani kote waliopo hapa Makao Makuu ya UN.”
Akitoa ushauri kwa vijana Sheila amewaeleza “Waweze kujitokeza na kuhudhuria mafunzo kama haya ili wawe na uwezo au uelekeo mpana kwa mafunzo yao ambayo wanayachukua.”
Sara Ole’ng
Kama ambavyo Sheila ameeleza kufanikiwa kushirikiana na watu kutoka kila pembe ya dunia, ndivyo hivyo ilivyokuwa kwa Sara Oleng ambaye baada ya mafunzo kwa vitendo mwaka 2023 hapa UN jijini New York Marekani akipata ajira katika shirika linaloendana na yale yanayotekelezwa na Umoja wa Mataifa.
Akiwa katika jimbo la Michigan Sarah anaeleza kuwa anafanya kazi katika shirika lisilo la kiserikali la Glimps of Afrika linalowasaidia wakimbizi waliochangua Marekani kama nchi yao ya pili.
“Tunafanya kazi nyingi za kuwasaidia wakimbizi, mfano kupata chakula hususan katika msimu hii wa sikukuu na hizi kazi zote naweza kusema zilianza wakati nipo katika Umoja wa Mataifa, kusaidia wakimbizi na kujua jinsi ambavyo watu hawa hutoka Afrika mpaka kufika hapa Marekani.”
Je nawe ungependa kuwa kama wao? Kama ni muhitimu wa chuo Kikuu kwa miaka isiyozidi miwili au unakaribia kuhitimu waweza kutembelea wavuti https://careers.un.org/ mara kwa mara na kuangalia iwapo kuna fursa ya mafunzo na ukaomba.