Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu vikwazo vya hivi karibuni vya Marekani dhidi ya majaji wawili wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), akisisitiza jukumu la mahakama hiyo katika kuhakikisha haki kimataifa.

“Katibu mkuu anaelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu uteuzi wa majaji wawili wa ziada wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ili kuadhibiwa chini ya amri ya utendaji, pamoja na wa mahakama nyingine za kimataifa za jinai na maafisa wa Umoja wa Mataifa,” msemaji wa Guterres, Farhan Haq alisema jana Alkhamisi katika mkutano na waandishi wa habari.

Huku akibainisha kwamba Umoja wa Mataifa na ICC ni “taasisi tofauti zenye mamlaka tofauti,” Farhan Haq amesisitiza kwamba Umoja wa Mataifa unaiona mahakama ya ICC kama “nguzo muhimu ya haki ya jinai ya kimataifa, na Katibu Mkuu anaheshimu kazi yake.”

Ameongeza kuwa: “Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia anasisitiza umuhimu wa kanuni ya msingi ya uhuru wa mahakama.” 

Mapema jana Alhamisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio alitangaza vikwazo dhidi ya majaji wa ICC, Gocha Lordkipanidze wa Georgia na Erdenebalsuren Damdin wa Mongolia, akiwatuhumu kwa eti “kuhusika moja kwa moja” katika “kulenga Israel kinyume cha sheria.”

Hapo awali, Marekani ilikuwa imewaadhibu maafisa wa mahakama ICC kwa kuidhinisha hati za kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Waziri wa zamani wa Vita, Yoav Gallant kwa kuhusika na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika Ukanda wa Gaza huko Palestina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *