Mwanautalii Al Barwani rasmi balozi wa utalii TanzaniaMwanautalii Al Barwani rasmi balozi wa utalii Tanzania

DAR ES SALAAM: MWANAUTALII na mtangazaji wa vivutio vya utalii kutoka Oman, Khalid Hamed Al Barwani, aliyesaidia kulitangaza kimataifa Shamba la Miti Sao Hill baada ya kuitembelea mwaka 2024, amekabidhiwa rasmi Ubalozi wa Hiari wa Utalii wa Tanzania katika hatua inayotarajiwa kuimarisha kampeni za kuitangaza nchi na kuongeza idadi ya watalii.

Ubalozi huo ulikabidhiwa na Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, ikiwa ni kutambua mchango wa Al Barwani katika kuitangaza Tanzania kupitia majukwaa ya kimataifa.

Al Barwani aliongoza kundi la Dream Team Explorers kutembelea Shamba la Miti Sao Hill mwaka 2024, ambapo walijionea vivutio mbalimbali vinavyopatikana katika eneo hilo, ikiwemo misitu ya kupandwa yenye mandhari ya kuvutia, mazingira ya kipekee ya asili pamoja na eneo la Mto Ruaha.

Ziara hiyo ilikuwa sehemu ya juhudi za kuitangaza Tanzania kama moja ya maeneo yanayoongoza kwa utalii wa asili na ikolojia, huku Sao Hill ikiendelea kujijengea nafasi kama kivutio kipya kinachovutia watalii wa ndani na wa kimataifa.

Baada ya kutembelea eneo hilo, Al Barwani na ujumbe wake walieleza kuvutiwa na uzuri wa Sao Hill na kuahidi kuendelea kulitangaza kupitia mitandao na majukwaa mbalimbali ya kimataifa, hatua iliyochangia kuongeza mwonekano wa kivutio hicho katika masoko ya utalii nje ya nchi.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi ubalozi huo, Mafuru alisema Serikali imeamua kumtambua Al Barwani kutokana na mchango wake katika kuitangaza Tanzania duniani, akieleza kuwa ubalozi huo ni sehemu ya mkakati wa kushirikisha watu mashuhuri na wadau wa kimataifa katika kuhamasisha utalii wa Tanzania.

Alisema mabalozi wa hiari wa utalii ni nguzo muhimu katika kufikisha taarifa za vivutio vya Tanzania kwa masoko mapya na kuongeza ushindani wa nchi katika sekta ya utalii duniani.

Uteuzi wa Al Barwani unatarajiwa kuipa nguvu kampeni ya kuitangaza Tanzania, hususan vivutio vya utalii wa misitu kama Shamba la Miti Sao Hill, na kuongeza idadi ya watalii pamoja na mapato yatokanayo na sekta hiyo, ambayo ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya fedha za kigeni nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *