Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP limesema linaongeza kasi ya msaada wa dharura wa chakula kufuatia kuongezeka kwa machafuko yaliyowalazimu mamia ya maelfu ya watu kuyahama makazi yao. Takribani watu 500,000 wamekimbia makazi yao katika jimbo la Kivu Kusini tangu mapigano yalipoanza mapema Desemba, huku vituo vya afya vikivamiwa, shule zikifungwa, na huduma za msingi zikikaribia kuporomoka.
WFP imesema inahitaji haraka dola milioni 67 ili kuendelea kutoa msaada kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo. Cynthia Jones, Mkurugenzi wa muda wa WFP nchini DRC amesema “Bila hatua za haraka mgogoro huu wa njaa uko hatarini kuongezeka kwa kasi”, akiongeza kuwa Familia zinazowahifadhi waliokimbia makazi, ambazo tayari zinakabiliwa na njaa kali, zinagawana chakula chao cha mwisho na hivyo kuwasukuma wote kuelekea kukata tamaa kabisa.”
wawakilishi wa kamati ya umoja wa Mataifa kuhusu Mateso wakizungumza na waandishi wa habari (Kutoka maktaba)
Kamati ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa leo imesema mjini Geneva kwamba imebaini kuwa Burundi iliwalipizia kisasi mawakili kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa, kinyume na Mkataba wa Kupinga Mateso.
Kamati hiyo ya Kupinga Mateso inasema mawakili wanne wa Burundi walinyang’anywa leseni za uwakili na mali zao kutaifishwa baada ya kushiriki katika mapitio ya rekodi ya haki za binadamu ya nchi hiyo mbele ya Umoja wa Mataifa.
Mjumbe wa Kamati hiyo, Todd Buchwald, amesema, “Nchi lazima zilinde, si kuwaadhibu, wale wanaotaka kushirikiana na vyombo vya kimataifa vya haki za binadamu.”
Kamati imeitaka Burundi kurejesha leseni za mawakili hao, kurudisha mali zao, na kuzuia vitendo kama hivyo siku zijazo.
Watoto 660,00 Gaza wamekosa fursa ya masomo sababu ya mgogoro unaoendelea
Gaza, Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema watoto wanaendelea kulipa gharama kubwa zaidi ya Athari za vita. Nyumba na shule zimeharibiwa, na kizazi kizima kinakua katika mazingira ya hofu na vurugu. UNRWA imeongeza kuwa watoto wanaendelea kuelezea matumaini yao kupitia michoro na nyimbo, wakibuni taswira ya madarasa yanayofunguliwa tena na nyumba zinazojengwa upya.
Licha ya uharibifu mkubwa, UNRWA inasisitiza kuwa kila mtoto ana haki ya kuishi, kujifunza na kuota ndoto za maisha bora, huku shirika hilo likiendelea kutoa elimu, huduma za afya na msaada wa dharura kwa mamilioni ya watu Gaza na katika eneo lote.
