Kamati hiyo imechapisha uamuzi wake leo baada ya kupitia ombi lililohusu kesi ya mawakili wanne wa Burundi waliowasiliana moja kwa moja na kamati hiyo mwaka 2016 wakati wa mapitio ya utekelezaji wa Burundi wa mkataba huo wa haki za binadamu.
Kamati imesema mawakili hao walichangia ripoti ya pamoja ya asasi za kiraia iliyowasilishwa kwa kamati, na watatu kati yao walisafiri hadi Geneva kushiriki mapitio ya nchi wakati wa kikao cha 58 cha Kamati.
“Asasi za kiraia zina jukumu muhimu sana katika mchakato wa kamati wa kupitia hali ya haki za binadamu ya nchi chini ya Kifungu cha 19 cha mkataba. Nchi zinapaswa kulinda, si kuadhibu, wale wanaotafuta kushirikiana na vyombo vya kimataifa vya haki za binadamu.” amesema Todd Buchwald, mjumbe wa Kamati hiyo.
Kwa mujibu wa wadai, walishiriki maandamano ya amani nchini Burundi mwaka 2015 kupinga uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza wa kuwania muhula wa tatu madarakani, ambao waliuona kuwa kinyume cha katiba.
Maandamano hayo yalizimwa kwa nguvu na mamlaka, huku vikosi vya usalama vikiwalenga waandamanaji na wapinzani wa kisiasa. Wadai wamelaani hadharani ukandamizaji huo wa kikatili na, kufuatia ukandamizaji uliotokea baadaye, walikimbia Burundi na kuishi uhamishoni kwa hofu ya usalama wao.
Balozi Elisa Nkerabirori, Mwakilishi wa Kudumu wa Burundi kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Geneva, Uswisi.
Burundi yagoma kushiriki mchakato
Kamati imebaini kuwa serikali ya Burundi imekataa kushiriki sehemu ya pili ya kikao cha siku mbili kilichopangwa, kama njia ya kupinga matumizi ya Kamati ya taarifa zilizowasilishwa na asasi za kiraia.
Siku hiyo hiyo, mwendesha mashtaka wa umma wa mahakama ya rufaa ya Bujumbura ameomba rasmi kuwavua wadai leseni za uwakili, hatua iliyochochea mashauri ya kisheria yaliyoishia kuwavua watatu kati yao leseni na kumsimamisha wa nne.
Kamati imeeleza wasiwasi kuwa hatua hizi zimekuwa za kulipiza kisasi katika barua ilizotuma tarehe 12 Agosti 2016 na 21 Februari 2017, ambazo Burundi haikujibu. Aidha, mwaka 2019, Rais wa mahakama ya juu na mwanasheria mkuu aliamuru kutaifishwa kwa mali za wadai hao.
Kwa kukosekana kwa maelezo yoyote kuhusu muda wa hatua hizo au ufafanuzi kutoka kwa Serikali husika, kamati imebaini kuwa imethibitishwa vya kutosha kuwa hatua hizo zimekuwa za kulipiza kisasi kwa sababu ya ushirikiano wa wadai na kamati, kinyume na kifungu cha 13 cha mkataba.
Buchwald amesema “Kamati imesisitiza tena kuwa nchi zote zina wajibu wa kujiepusha na vitisho au kulipiza kisasi dhidi ya watu wanaotafuta kushirikiana na Kamati na kushiriki kwa nia njema katika taratibu za utoaji taarifa na malalamiko chini ya mkataba,”
Kamati imeihimiza Burundi kuchukua hatua za haraka kurekebisha ukiukwaji huo. Imeitaka serikali kurejesha leseni za uwakili za wadai, kufuta marufuku zote za kitaaluma na kurejesha haki zao za umiliki wa mali. Pia imeomba Burundi kutoa fidia kamili kwa wadai na kuhakikisha kuwa ukiukwaji kama huo hautokei tena siku zijazo.