Akilihutubia Baraza hilo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani hii leo jumanne 23 Desemba 2025 jioni , Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Kisiasa na Ujenzi wa Amani na Operesheni za Amani, Khaled Khiari, amesema operesheni hizo zimeongezeka tangu kikao cha mwisho cha Baraza kuhusu suala hilo kilichofanyika tarehe 10 Oktoba 2025.

Kwa mujibu wa Khiari, serikali ya Marekani imeeleza kuwa hatua hizo ni sehemu ya “mgogoro wa silaha usio wa kimataifa” dhidi ya biashara ya dawa za kulevya, ikirejea Ibara ya 51 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Rais wa Marekani, Donald Trump, amenukuliwa akisema atatumia “nguvu zote za Marekani” kutokomeza magenge ya dawa za kulevya bila kujali yanakofanyia shughuli zao.

Serikali ya Venezuela imepinga maelezo hayo na kueleza kuwa hatua za Marekani ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa. Katika mawasiliano rasmi kwa Baraza la Usalama, Caracas imeituhumu Marekani kukiuka marufuku ya matumizi au vitisho vya nguvu, pamoja na kukiuka uhuru na uadilifu wa mipaka ya Venezuela.

Khiari amesema Marekani imeendelea kushambulia vyombo vya majini vinavyoshukiwa kusafirisha dawa za kulevya katika eneo la kusini mwa Bahari ya Karibea na Mashariki mwa Pasifiki. Kulingana na taarifa za mamlaka za Marekani, watu wasiopungua 105 wamefariki tangu tarehe 2 Septemba katika operesheni hizo.

Amelikumbusha Baraza la Usalama kuwa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu ameeleza mashambulizi hayo ya angani kuwa yanakinzana na sheria za kimataifa, akisisitiza haja ya uchunguzi huru na wa uwazi.

Khiari pia amesema kuongezeka kwa hatua hizo kumeambatana na kufungwa kwa anga ya Venezuela, kunyakuliwa kwa meli za mafuta, vikwazo vipya, na kuongezeka kwa wasiwasi wa nchi kadhaa kuhusu kuimarika kwa matumizi ya kijeshi katika eneo hilo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa mazungumzo ni njia pekee ya kuepusha kuyumba zaidi kwa hali na mateso ya kibinadamu katika eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *