Viongozi wa Muungano wa Mataifa ya Sahel (AES), kundi linalojumuisha Mali, Burkina Faso na Niger, umeanzisha shirika jipya la habari lenye makao yake makuu katika mji mkuu wa Mali, Bamako.

Televisheni ya AES inasemekana kuwa hatua muhimu katika malengo ya kutoa taarifa huru kwa kundi hilo la Afrika Magharibi, na limeelezwa kuwa chombo rasmi cha kukabiliana na upotoshaji wa taarifa na kuimarisha simulizi ya kanda hiyo.

Televisheni hiyo ilizinduliwa siku ya Jumanne katika hafla iliyohudhuriwa na Rais wa Mali Jenerali Assimi Goita, Rais wa Burkina Faso Kapteni Ibrahim Traore na Rais wa Niger Jenerali Abdourahamane Tiani waliokutana mjini Bamako kwa mkutano wa siku mbili kutathmini mwaka mmoja wa muungano wa AES.

Mali, Burkina Faso na Niger zilijiondoa rasmi katika Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) Januari 2025 kufuatia mchakato wa mwaka mzima.

Taarifa kutoka ofisi ya rais wa Burkina Faso imesema, viongozi hao watatathmini ripoti ya utekelezaji, kufanya maamuzi ili kuangazia mafanikio na kushughulikia changamoto kubwa zinazokabili AES.

Hatua zilizopigwa na AES hivi karibuni ni pamoja na uzinduzi wa kikosi cha pamoja cha AES wiki iliyopita (FU-AES) ambacho kina makao makuu yake mjini Niamey, Niger. Kikosi hicho kinategemewa kuwa na wanajeshi karibu 5,000 kukabiliana na makundi yenye silaha.

Halikadhalika, muungano huo umeasisi Benki ya Uwekezaji na Maendeleo (BCID-AES), kwa mtaji wa kwanza wa karibu dola milioni $900, kwa lengo la kupunguza utegemezi wa ufadhili kutoka nje kwa kuimarisha miundombinu, nishati na miradi ya kilimo.

AES, yenye kujumuisha watu milioni 78, inaendelea kuunganisha nchi wanachama katika masuala ya usalama, uchumi na mawasiliano ikiwa ni ishara ya kuelekea kujisimamia na kujitegemea wenyewe katika eneo la Sahel…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *