Familia ya mwigizaji mkongwe wa Hollywood, Bruce Willis, imetangaza kutoa ubongo wa mwigizaji huyo kwa ajili ya utafiti wa kisayansi atakapofariki dunia, hatua hiyo itachukuliwa kwa lengo la kusaidia tafiti za ugonjwa wa frontotemporal dementia (FTD) anaougua.
Bruce Willis, mwenye umri wa miaka 69, alitangaza kuachana rasmi na uigizaji mwaka 2022 baada ya awali kugundulika kuwa na tatizo la aphasia, hali iliyoathiri uwezo wake wa kuzungumza na kuwasiliana. Baadaye, mwaka 2023, aligundulika kuwa na ugonjwa wa frontotemporal dementia (FTD).
Ugonjwa wa frontotemporal dementia huathiri zaidi sehemu za mbele na za pembeni za ubongo, hali inayosababisha mabadiliko katika haiba, tabia, uwezo wa kufanya maamuzi na lugha.
Mke wa mwigizaji huyo, Emma Heming-Willis, ameeleza kuwa uamuzi huo ni miongoni mwa maamuzi magumu zaidi kihisia ambayo familia imewahi kuyafanya. Hata hivyo, alisisitiza kuwa kama familia wamepitia changamoto nyingi lakini kutoa msaada wa ubongo wa mume wake kwa ajili ya utafiti kumewapa tumaini na faraja.
Katika taarifa mbalimbali walizotoa awali, familia ya Willis imekuwa ikisisitiza umuhimu wa jamii kuelewa changamoto wanazopitia wagonjwa wa FTD, ikieleza kuwa ugonjwa huo hubadilisha si tu maisha ya mgonjwa bali pia ya watu wanaomzunguka.
Aidha wataalamu wa afya wanasema uchunguzi wa ubongo baada ya kifo utatoa fursa ya kipekee ya kuchambua mabadiliko ya seli za neva ambayo hayawezi kubainika kwa urahisi mtu akiwa hai. Kupitia uchunguzi huo, wanasayansi watafanikiwa kupata ushahidi wa moja kwa moja unaosaidia kuboresha utambuzi wa ugonjwa, mbinu za matibabu na hata tafiti za kuzuia magonjwa ya aina hiyo.
Bruce alianza kutambulika kupitia tamthilia ya Moonlighting (1985-1989) akicheza kama David Addison Jr ambapo filamu hiyo ilimfanikisha kunyakua tuzo ya Emmy na Golden Globe.
Pia ameonekana katika filamu mbalimbali ikiwamo Die Hard, Pulp Fiction (1994), 12 Monkeys (1995), The Fifth Element (1997), Armageddon (1998), The Sixth Sense (1999), na Glass (2019) huku filamu ya mwisho kuonekana ikiwa ni ‘Assassin’ iliyotoka Machi 2023.