
Waziri mmoja wa utawala wa Kizayuni wa ameishambulia Qatar kwa maneno makali na kutamba kuwa shambulio la miezi ya hivi karibuni lililofanywa na Israel nchini Qatar lilikuwa ni “hatua sahihi” iliyokuwa ya lazima kuchukuliwa.
Shirika la Habari la Mehr limeinukuu tovuti ya gazeti la Al-Quds Al-Arabi ikitangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, waziri wa uhamiaji wa Israel, Amichai Chikli kutoka chama cha Likud ameishambulia vikali kwa maneno Qatar akisema kwamba, jaribio la Israel nchini humo dhidi ya viongozi wa HAMAS lilikuwa sahihi na amepuuza madai kuwa waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu aliomba msamaha kwa Qatar kwa shambulio hilo la kigaidi.
Akihojiwa na kituo cha redio cha Kizayuni cha “103FM,” Chikli amedai kuwa Qatar ni “mji mkuu wa kundi la Ikhwanul Muslimin.” Alitamba kwa kusema kuwa, Israel ilifanya jambo sahihi kuushambulia mji mkuu wa Qatar Doha hivi karibuni dhidi ya viongozi wa Hamas na ametaka mashambulizi ya namna hiyo yaendelee.
Kauli hizi zimekuja baada ya jeshi la Israel kufanya shambulio la anga huko Doha tarehe 9 Septemba mwaka huu na kuua baadhi ya wanachama wa HAMAS na maafisa wa Qatar kujeruhi wengine kadhaa. Dunia ilikemea vikali jinai na ugaidi huo wa Israel huku Qatar ikisema kuwa jinai hiyo ilikiuka haki ya wazi ya kujitawala nchi hiyo ya Kiarabu.
Kama tulivyotangulia kusema, shambulio hilo la kigaidi la Israel katika ardhi ya Qatar lililaaniwa vikali duniani na hasa katika Ulimwengu wa Kiarabu huku wote wakisema kuwa, jinai hiyo ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na uhuru wa kujitawala nchi ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa.