Hilo ni onyo kali lililotolewa leo na WHO wakati wa msimu huu wa sikukuu, ambapo matumizi ya pombe huongezeka na hivyo kuongeza majeraha yanayoweza kuzuilika.

Kwa mujibu wa takwimu mpya za WHO kanda ya Ulaya, karibu vifo 145,000 vya majeraha mwaka 2019 vilihusishwa moja kwa moja na matumizi ya pombe. Sababu kuu ni pamoja na kujidhuru, ajali za barabarani na kuanguka.
WHO inasema hakuna sababu nyingine ya kisaikolojia inayochangia vifo vya majeraha kwa kiwango kikubwa kama pombe.

Carina Ferreira-Borges, Mshauri wa Kikanda wa WHO barani Ulaya kuhusu masuala ya pombe, anafafanua kwamba “Pombe ni kinywaji chenye sumu ambayo haisababishi tu aina saba za saratani, bali pia huharibu uwezo wa kutoa maamuzi sahihi, hupunguza uwezo wa kujizuia, hupunguza kasi ya kuchukua hatua, huharibu uratibu wa mwili na kuchochea tabia ambazo ni hatarishi.”

Matumizi ya mihadarati miongoni mwa vijana barubaru ni tatizo kubwa kote duniani

© UNICEF/Giacomo Pirozzi

Matumizi ya ulevi miongoni mwa vijana barubaru ni tatizo kubwa kote duniani

Pombe chachu ya vurugu

WHO inasema pombe ni miongoni mwa vichochezi vikubwa vya vurugu na uchokozi.

Mwaka 2019, zaidi ya asilimia 40 ya vifo vinavyotokana na vurugu za kijamii katika ukanda huo wa Ulaya vilihusishwa na pombe. Wanawake na watoto ndio waathirika wakubwa zaidi.

Melanie Hyde, Afisa wa Kiufundi wa Masuala ya Jinsia, Usawa na Haki za Binadamu wa WHO katika Kanda ya Ulaya, anasema kinga inawezekana.

“Matumizi mabaya ya pombe kwa wanaume ni sababu hatarishi katika kutekeleza vurugu dhidi ya wenzi wao wa ndoa. Hii ni sababu inayoweza kurekebishwa kupitia juhudi za kuzuia unywaji wa pombe.”

media:entermedia_image:6e90d91a-250f-48d3-979b-250b8e2b25a6

© WHO/Alex Plonsky

Chupa za mvinyo kwenye dula la kuuza pombe

Hatari kubwa kwa vijana

Kwa mujibu wa shirika hilo la afya vijana wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi ya majeraha yanayohusiana na pombe.

Jonathon Passmore, Mshauri wa Kikanda wa WHO barani Ulaya kuhusu usalama barabarani, anaonya kwamba  “Vijana wako katika hatari kubwa ya unywaji wa pombe kupindukia kwa muda mfupi. Mtindo huu huongeza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa ajali za barabarani, kuzama majini, vurugu na kujidhuru.”

Nini kifanyike

WHO inazitaka serikali kuongeza kodi ya pombe, kudhibiti upatikanaji wake, kupiga marufuku matangazo makali na kuimarisha sheria za kuendesha magari baada ya kunywa pombe hatua ambazo zinaweza kuokoa makumi ya maelfu ya maisha kila mwaka.

Kadri msimu wa sikukuu unavyoanza, WHO inawakumbusha wananchi kuwa kunywa kwa kiasi, kujua wakati wa kuacha na kutoendesha gari baada ya kunywa pombe kunaweza kuzuia vifo na majeraha  na kuhakikisha sherehe salama kwa wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *