Katika hospitali ya Al- Shifa iliyoko mjini Gaza, moja ya hospitali chache zilizosalia baada ya miaka miwili ya vita na ni tegemeo la wagonjwa wengi.

Ndani ya hospitali hii katika chumba cha wagonjwa mahututi ambao ni watoto au Pediatric ICU amelala mtoto Sama Abu Ajwa akiwa amewekewa mipira usoni, kifuani na mikononi. Mtoto huyu mwenye umri wa miezi nane pekee hapa duniani anasumbuliwa na matatizo ya figo.

Balqees Abu Ajwa ni mama wa mtoto huyo, akiwa pembeni ya mtoto wake akimuangalia kwa huzuni anasema hawajaweza kupata matibabu wanayohitaji. “Mtoto wangu huyu wa kike ni mgonjwa, ana shida ya figo. Mipaka ya kuingia Ukanda wa Gaza imefungwa na vifaa vya matibabu ni vichache. Vifaa vya matibabu ambavyo vinaweza kumsaidia mwanagu kuendelea kuishi havipatikani. Mtoto wangu amekuwa katika hali hii kwa siku 20; amechoka, na mimi nakuja hapa hospitali kumuangalia kila siku. Hivi sasa ninaogopa kumpoteza kwa sababu matibabu hayapatikani. Tulikamilisha taratibu za rufaa ya kimatibabu nje ya Ukanda wa Gaza kwa ajili ya matibabu yake, lakini hadi sasa hakuna kilichotokea, licha ya kupata rufaa kwa haraka kutokana na hali yake ya kiafya lakini hadi sasa, bado tunasubiri. Hali yake inazidi kuwa mbaya siku baada ya siku, viwango vyake vya damu vinazidi kupungua, na viashiria vya figo lake kushindwa kutenda kazi vinaongezeka.”

Katika chumba hicho cha watoto walio mahututi anaingia Daktari Rifaat Jundiya ambaye anawaangalia na kuwapima wagonjwa. Akuzungumzia hali ilivyo anasema “Hali ya kiafya katika Ukanda wa Gaza ni ngumu sana kutokana na ukosefu wa wafanyakazi wa afya wa kutosha pamoja na uhaba mkubwa wa vifaa vya matibabu. Kwa mfano, katika kitengo cha wagonjwa mahututi tunahitaji haraka mashine ya X-ray inayoweza kuhamishika, kutokana na ugumu wa kuwahamisha wagonjwa waliounganishwa na machine za kuwasaidia kupumua na hivyo kushindwa kuwapelekwa hadi idara ya radiolojia katika jengo lingine.”

Gazeti The World Health Organization linaripoti kwamba hospitali ya Al Ahli huko Gaza ilionyesha kwamba vifaa vya kitiba na vifusi viliharibiwa baada ya kushambuliwa.

Umoja wa Mataifa

Juhudi zinazofanywa na UN

Tangu mwezi Oktoba 2023, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO na washirika wake wamefanikiwa kuwahamisha zaidi ya wagonjwa 10,600 kutoka Ukanda wa Gaza wenye hali mbaya ya kiafya, wakiwemo zaidi ya watoto 5,600, kila mmoja akihitaji matibabu muhimu ya hali ya juu. Hata hivyo, wagonjwa wengi zaidi bado wako Gaza wakisubiri kuhamishwa ili kupata huduma inayofaa ya afya.

WHO imesema kwamba kwamujibu wa Wizara ya Afya, wagonjwa 1,092 wamefariki wakati wakisubiri kuhamishwa kimatibabu kati ya Julai 2024 na Novemba 28, 2025. Hata hivyo, takwimu hii huenda hairipotiwi vya kutosha.

WHO inatoa wito kwa nchi zaidi kufungua milango kwa kupokea wagonjwa kutoka Gaza, na kwa ajili ya kuhamishwa kimatibabu hadi Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Yerusalemu Mashariki, ili kurejeshwa. Maisha yanategemea hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *