Ukweli una sifa moja tu, kwamba hata ukiukataa, haugeuki kuwa uongo. Hivyo hakuna ubishi kuwa mwaka 2025 taifa letu limepitia katika majaribu makubwa na ili kuponya majeraha, suluhisho pekee ni kuondoa chuki na kutafuta maridhiano.

Kuna msemo wa Kiswahili usemao: ‘Panapofuka moshi, chini kuna moto,’ kwa sababu cheche za kile ambacho taifa limekipitia, zilianza kuonekana miaka kadhaa nyuma na Oktoba 29, 2025 ilifikia tu kilele chake.

Kwa tunaojua kusoma alama za nyakati, tulifahamu kuwa kuna nyakati za giza zinakuja kama haki haitatamalaki nchini ili imzae mtoto amani, badala yake tukaimba amani bila kuelewe kwamba bila haki hakuna amani.

Bahati mbaya sana, hata baada ya yaliyotokea Oktoba 29, 2025, baadhi ya viongozi hawafahamu ni kitu gani kimelifanya taifa lifikie hapo na wananyoosha kidole kwa wengine.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema: “Hatuwezi kutatua matatizo yetu kwa kujidanganya eti hayapo,” na mimi naona kabisa hatutaki kutafuta mahali tulipojikwaa na kuanguka, tunatafuta tulipoangukia.

Hivi ni kweli kuna Mtanzania asiyefahamu kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa 2019, uchaguzi mkuu 2020 na uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 ulizalisha kitu kinachitwa chuki na ulilalamikiwa kuwa haukuwa huru, wa haki wala wa kuaminika?

Ni katika chaguzi hizo umma wa Watanzania ulianza kushuhudia aina mpya ya demokrasia ya vyama vingi, wagombea kutoka vyama vya upinzani wanaenguliwa kwa maelfu na mawakala wao kutimuliwa kwenye vituo vya kupigia kura?

Hivi ni kweli hatufahamu kuwa ni katika chaguzi za serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu 2020 ndio tulishuhudia kauli za ubaguzi kutoka kwa baadhi ya wanasiasa kuwa usipochagua mgombea wa CCM maendeleo hayatakuja?

Walieneza sumu hiyo wakijua kuwa ibara ya 3(1) ya Katiba ya nchi inaeleza kuwa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia inayofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa na ibara yake ya 13(4) inakataza mtu yeyote kubaguliwa na mamlaka za nchi.

Katiba imefafanua neno ubaguzi maana yake ni kutimiza haja, haki au mahitaji mengineyo kwa watu mbalimbali kwa kuzingatia utaifa wao, kabila, pahala walipotokea, maoni yao ya kisiasa, rangi, dini, jinsia au hali yao ya maisha.

Ubaguzi huu haukuishia hapo, ni kipindi hicho cha miaka mitano au Zaidi, ndio tuliona Watanzania tukigawanywa kiitikadi, kwamba tatizo la kijamii linalomkuta kiongozi au mwanachama wa chama cha upinzani basi wana CCM wanakaa mbali.

Hebu tujiulize, ni viongozi gani wa kitaifa ukimuondoa makamu wa Rais ambaye sasa ni Rais, Samia Suluhu waliomjulia hali Tundu Lissu, wakati huo akiwa mbunge wa Singida Mashariki, alipopigwa risasi na kulazwa kule Nairobi, kama wapo wanahesabika na hawakutaka kufahamika.

Sote tunafahamu moto unapowaka ukauongezea mafuta ndio unawaka zaidi badala ya kuuzima, hivi ndivyo unavyoweza kuelezea matukio ya utekaji, kupotea kwa watu na mauaji yalivyokoleza chuki dhidi ya Polisi na Serikali kwa ujumla.

Matukio ya watu kukamatwa kiholela hususan wakosoaji wa Serikali, wanasiasa na wanaharakati, yanayodaiwa kufanywa na Jeshi la Polisi na vyombo vingine vyenye mamlaka ya ukamataji, nayo yalisambaza sumu hiyo ya chuki.

Kwa hiyo hatuna sababu ya kutafuta mchawi kwa nini vijana wa kizazi cha Gen Z walitangaza kuandamana kwa amani Oktoba 29, 2025 lakini maandamano hayo yakazua vurugu, mauaji ya raia, majeruhi na kuharibiwa kwa mali.

Lakini kuna jambo lingine ambalo limezidisha hasira, chuki na roho ya visasi dhidi ya maofisa wa vyombo vya dola, nalo ni miili ya baadhi ya waliouawa katika vurugu hizo za Oktoba 29 kutopatikana popote katika hospitali zetu.

Kidonda cha ndugu waliopoteza ndugu zao kutopata maiti za ndugu zao ili wawazike kwa heshima au ambao wametoweka, basi wajulikane wako wapi, wako hai au wamekufa, hakiwezi kupona kirahisi kwa matamko wala kujifanya kama hakijatokea.

Tunaweza kuwalaumu Watanzania wanaoishi nje ya nchi kwa kuratibu na kuhamasisha maandamano mitandaoni, lakini tujiulize kulitoka matamko mangapi ya kuonya juu ya maandamano hayo? Kwa nini waandamanaji hawakuyasikiliza wala wao kusikilizwa?

Hii inathibitisha kama nilivyosema ukweli una sifa moja tu, kwamba ukiukataa haugeuki kuwa uongo, kwamba ni kiashiria kibaya kuwa kuna pengo kubwa kati ya raia na viongozi wa kisiasa. Hawawaamini na hawawasikilizi.

Tunatokaje hapa?

Kwanza ni lazima watawala wakubali kuwa kama taifa kuna tatizo, wakiri na kutubu kuwa kulikuwa na mauaji ya raia wasio na hatia na kuna waliojeruhiwa ambao hawakuwa hata kwenye maandamano. Tukiri kwanza hili.

Pili, ni lazima tuwe wazi kwamba waathirika ambao wala hawakuwa kwenye maandamano wala kufanya vitendo vya jinai kama wizi, wanapaswa kutambuliwa na kulipwa fidia.

Lakini inapaswa kuunda Tume ya Ukweli na Maridhiano (TRC) kama iliyoundwa Afrika Kusini mwaka 1995, kufuatia kumalizika kwa ubaguzi wa rangi ambayo ilianzishwa chini ya Sheria ya Ujenzi wa Umoja wa Kitaifa na Maridhiano namba 34 ya 1995.

Tume hii ililenga kutoa jukwaa (platform) kwa waathiriwa kueleza madhila waliyoyapitia wakati wa zama za ubaguzi wa rangi iliyodumu kati ya mwaka 1960 na mwaka 1994 na wahalifu kukiri makosa yao na kuomba msamaha.

Kulingana na takwimu zilizopo, Tume hii ilipokea maelezo zaidi ya 21,000 kutoka kwa waathirika na kusikiliza ushuhuda wa watu 2,000 kwa njia ya wazi na Tume ilitoa msamaha kwa watu 849 walioshiriki au kuhamasisha uhalifu kipindi hicho.

Afrika Kusini sio nchi pekee iliyowahi kuunda Tume za aina hii, hata Gambia iliwahi kuunda tume kama hiyo mwaka 2017 kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu katika kipindi cha utawala wa Yahya Jammeh mwaka 1996 hadi 2017.

Ghana nayo iliwahi kuunda tume kama hiyo mwaka 2002 kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu na hata jirani zetu Kenya waliunda tume kama hiyo mwaka 2008 kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu na makosa ya uhujumu uchumi.

Nchi nyingine zilizowahi kuunda Tume za Maridhiano au zinazofanana na ya Afrika Kusini ni Liberia (2005), Mauritius (2009), Morocco (2004), Rwanda (1999), Sierra Leon (2000), Togo (2009) na Tunisia 2014) hivyo Tanzania hatutakuwa wa kwanza.

Tume hizi zilifanya kazi kubwa ya kurejesha umoja na maridhiano na kwa kuwa Rais Samia alishaahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu 2025 kuwa ndani ya siku 100 ataunda Tume ya Maridhiano, sisi raia tunahesabu na zimebaki siku 51.

Ninatamani Serikali ifanye utafiti (hata mimi wakiniomba nitafanya), kupitia mitandao ya kijamii, kuangalia michango hasi katika kila andiko linalowekwa na kiongozi iwe ni X (Twitter), Instagram au Facebook.

Kwa nini utafiti huo ni muhimu? Kiwango cha chuki kinachoonyeshwa katika mitandao ya kijamii hakimithiliki tena, huko ndiko mamia na maelfu ya wachangiaji wanafurahia vifo vya viongozi na kuwaombea wengine mabaya.

Hili eneo si la kupuuza hata kidogo, ukizinghatia utumiaji wa intaneti umefikia watu milioni 56.3, kwa mujibu wa ripoti ya takwimu ya sekta ya nawasiliano kwa robo ya mwaka inayoishia Septemba 2025, iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Kwa hiyo kama Nyerere alivyowahi kusema tusitatue matatizo yetu kwa kujifanya hayapo, ni muhimu sana viongozi wetu wakajishusha chini na kukubali tuna tatizo kama Taifa, lakini tukiendelea kushapaza shingo hatutatoka hapa tulipo.

Ndiyo maana nasema mwaka 2026 uwe ni mwaka wa kuondoa sumu kali ya uhasama na ulipizaji visasi inayolitafuta taifa letu na tutumie mwaka huo mpya kutafuta maridhiano ya kweli na tutafanikiwa tukikiri na kuukubali ukweli.

Tusipofanya hivyo tunaweza kujikuta miaka mitano yote ya Serikali ya awamu ya sita ikawa na hekaheka za maandamano na kuingia katika migogoro ya kidiplomasia na nchi wahisani, ambao wanaweza hata kutuwekea vikwazo.

0656600900

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *