Uwanja wa Ndege wa Sabiha Gökçen, ambao ni kituo cha usafiri wa anga upande wa Asia wa jiji la Istanbul, ulihudumia abiria milioni 44.2 kati ya Januari na Novemba, na kuvunja rekodi ya mwaka uliopita ya abiria milioni 41.4.
Waziri wa Uchukuzi na Miundombinu wa Uturuki, Abdulkadir Uraloğlu, alisema Alhamisi kuwa njia mpya ya ndege, iliyofunguliwa Desemba 2023 ili kuruhusu ndege kubwa kutua, imechangia kwa kiasi kikubwa kufikiwa kwa rekodi hiyo.
Taarifa hiyo ilitolewa katika maadhimisho ya miaka miwili tangu njia hiyo mpya ya ndege ianze kufanya kazi.
Uraloğlu alisema kuwa, pamoja na njia hiyo mpya, miundombinu mingine kama njia za kupitisha ndege (taxiway), maeneo ya maegesho ya ndege zenye uwezo mkubwa na mizigo, mnara wa kudhibiti safari za ndege, pamoja na majengo ya kisasa, vimeongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa uwanja wa ndege wa Sabiha Gökçen kuhudumia safari za anga.
Mwaka 2023, jumla ya abiria milioni 33.7 walihudumiwa kwenye safari za ndani na za kimataifa kati ya Januari na Novemba.