Katika ujumbe wake kwa mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa Jumuiya za Wanafunzi wa Kiislamu barani Ulaya, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: “Taifa la Iran kwa kutumia uwezo wake linaweza kusimama na kutoa wito wa thamani za Kiislamu kwa walimwengu kwa sauti kubwa kuliko wakati mwingine wowote.”
Katika ujumbe wake kwa mkutano wa 59 wa kila mwaka wa Umoja wa Jumuiya za Wanafunzi wa Kiislamu barani Ulaya mapema leo Jumamosi, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameangazia jukumu la vijana wa Iran katika kuzima mashambulizi makubwa ya jeshi la Marekani na “kitoto chake cha kuaibisha” katika eneo, akimaanisha utawala haramu wa Israel.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, amesema mashambulio makubwa ya jeshi la Marekani na mwanaharamu wake katika eneo la Asia Magharibi yalishindwa kutokana na ubunifu, ushujaa na kujitolea kwa vijana wa Iran ya Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amesema katika ujumbe wake huo: “Wapendwa Vijana! Mwaka huu, nchi yenu, kutokana na imani, umoja na kujiamini, imepata hadhi na uzito mpya duniani. Uvamizi mkubwa wa jeshi la Marekani na kijitoto chake cha kuaibisha katika eneo hili ulishindwa kutokana na ubunifu, ushujaa na kujitolea kwa vijana wa Iran ya Kiislamu”.
Ameongeza kuwa: Imethibitishwa kwamba taifa la Iran, kwa kutumia uwezo wake, chini ya kivuli cha imani na matendo mema, na katika kukabiliana na mabeberu waovu, linaweza kusimama kidete na kutoa wito wa thamani za Kiislamu kwa ulimwengu kwa sauti kubwa zaidi kuliko hapo awali.
Kadhalika Ayatullah Khamenei amesema kuwa, sababu kuu ya mkanganyiko wa mataifa ya kibeberu si mpango wa nyuklia wa Iran, bali ni msimamo wa nchi hii dhidi ya utaratibu usio wa kiadilifu na wa kiimla wa kimataifa na hatua yake ya kuanzisha mfumo wa kitaifa na kimataifa wenye msingi wa haki na uadilifu.
Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kikao cha kila mwaka cha Umoja wa Jumuiya za Wanafunzi wa Kiislamu barani Ulaya unasisitiza mambo kadhaa muhimu. Katika ujumbe wake, kushindwa kwa uvamizi wa Marekani katika eneo hilo kunahusishwa na hatua, ujasiri na kujitolea mhanga kwa vijana wa Iran. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi anasisitiza kuwa, taifa la Iran limeweza kusimama dhidi ya madola jeuri na ya kimabavu kwa imani na matendo mema.
Ayatullah Khamenei amesisitiza juu ya suala hili pia kwamba, licha ya kuweko ghamu na huzuni kubwa ya kuuawa wanasayansi kadhaa, makamanda wa jeshi na raia wengine lakini hilo halijaweza na halitaweza kusimamisha harakati ya vijana wa Iran wenye hima kubwa, akibainisha kwamba familia za mashahidi hawa zenyewe ziko mstari wa mbele katika harakati hiyo.
Kadhalika Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amesema kuwa, Jamhuri ya Iran ya Kiislamu ni mbeba bendera ya kukabiliana mfumo wa kibeberu na mlinganiaji wa kuwepo mfumo wa kiadilifu wa Kiislamu ulimwenguni; suala ambalo kwa mujibu wake, ndilo sababu kuu ya mkanganyiko wa mataifa makubwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amesisitiza mara kwa mara kwamba wito mkubwa wa Iran ya Kiislamu hauko katika masuala ya kiufundi na kiuchumi pekee, bali ni kubuni kiigizo kipya ca kimataifa, ambacho kimejikita katika uadilifu na thamani za Kiislamu, na hii imesababisha wasiwasi na miitikio hasi kutoka kwa madola ya kibeberu duniani.
Kiongozi wa Mapinduzi pia anaitambulisha Iran kama mwanzilishi wa mageuzi ya kimataifa; mageuzi ambayo yanalenga kubadilisha utaratibu uliopo wa kibeberu na usio wa kiadilifu na nafasi yake kuchukuliwa na mfumo wa Kiislamu uliojengeka juu ya misingi ya uadilifu, umaanawi na mamlaka ya kujitawala mataifa.
Hapana shaka kuwa, mtazamo wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusiana na mfumo wa uadilifu wa ulimwengu wa Kiislamu ni mpango wa kimkakati ambao unaifanya Iran kuwa mbeba bendera ya kukabiliana na ubeberu na unasisitiza nafasi ya vijana katika kufanikisha mabadiliko haya. Mtazamo huu sio tu kwamba, unaathiri sera ya kigeni ya Iran, lakini pia unaweza kuhamasisha harakati za kijamii na za wanafunzi ulimwenguni kote.