DAR ES SALAAM: MKUU wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo ameliagiza Jeshi la Polisi kupitia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, ACP Yustino Mgonja kutumia utaalamu na timu yake kuwakamata mara moja kundi la watu waliofanya mauaji ya mwananchi Mzee Salehe Idd Salehe.

Salehe ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Zavala Kata ya Buyuni wilaya ya Ilala Dar es salaam alivamiwa akiwa nyumbani kwake na kundi la wahalifu Desemba 4,2025 Majira ya saa 11:00 alfajiri na alifariki siku hiyo akiwa njiani kuelekea Hospitali ya Amana.

Mpogolo alitoa agizo hilo kwenye Mkutano wake na Wananchi uliofanyika katika Mtaa wa Zavala mara baada kupata taarifa za uvamizi wa kinyama aliyofanyiwa mzee huyo akiwa nyumbani kwake na baadaye kupelekea kifo chake.

Akizungumza katika mkutano huo Mpogolo alisema Mzee Salehe katika Maisha yake amekuwa mzalendo wa kweli kwa kupigania maeneo ya wazi ya Serikali mfano Shule, Masoko na Vituo vya Afya yasichukuliwe na genge la Wahalifu wanaouza maeneo hayo ya wazi ya Viwanja vilivyopimwa na Serikali katika Programu ya Viwanja Elfu 20 Kata ya Buyuni kati ya miaka ya 2003/2005.

“Kamanda RPC wa Ilala nakuagiza tumia vyombo vyako na utaalamu wako na ninahakika unaweza kuakikisha mnawakamata watu wote waliofanya mauaji haya na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Kwa kuwa wauaji hawa inaelekea wanao mtandao mkubwa wa kiuhalifu katika eneo letu la Wilaya za kipolisi za Chanika na Ukonga,”alisema Mpogolo.

Akitoa agizo hilo Mpogolo alisema Jeshi la Polisi chini ya ACP Mgonja lina mfumo na nyenzo imara sana za uchunguzi na ukamataji, hivyo aliwaomba wananchi wampatie imani na chombo cha Polisi kifanye uchunguzi na kikamate haraka na kuweza kuleta imani kwa wananchi juu ya usalama wao na usimamizi wa sheria.

Pia Mpogolo alimwagiza Mkurugenzi wa Jiji kupitia Idara ya Mipango Jiji kuendelea kuyatambua na kuyarejesha maeneo yote wazi ya huduma za jamii yaliyolipiwa na kutengwa na serikali. Pia washirikiane na Jeshi la polisi kubaini genge la Wahalifu wa viwanja vya Umma wanao uza kwa watu wasiojua.

Katika hatua nyingine mkutano wa Mpogolo na wakazi wa Mtaa wa Zavala, Buyuni aliofanya hivi karibuni akiwa katika ziara yake ndogo ulipeleka matumaini na faraja kwa wakazi wa Zavala na wote wanaopambania na kulinda maeneo ya wazi yasichukuliwe na wahalifu.

Awali, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Zavala, Faridu Rashidi alisema katika Mtaa wa Zavala Kata ya Buyuni kwa sasa wananchi wanakaa kwa hofu kubwa kwa kuhofia kundi la watu wasiojulikana ambao wamefanya mauaji hayo.

Rashid alisema kwa sasa wananchi wanaogopa kuongea kutokana na vitendo hivyo na wengine wamekimbia makazi yao hasa wale waliokuwa wanatetea maeneo ya huduma za jamii yasiuzwe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *