Desemba 26, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Ware House uliopo Masaki mmoja kati ya pambano kumi yaliopigwa usiku huo lilikuwa kati Mtanzania, Hamadi Furahisha dhidi ya Hannock Phiri ‘Kumbakumba’ kutoka Malawi.

Pambano hilo ambalo limefanyika chini ya promotioni ya Peak Time Media limekuwa la aina yake kutokana, Phiri kuwaduwaza mabondia mara zote anapokuwa akipambana nao nchini kutokana na mtindo wake wa kupigana bila fomula yaani kuvamia kwa vurugu ili aweze kushinda.

Phiri anafahamika  na Watanzania waliokuwa na uwezo wa kucheza kwa fujo na siyo mchezo wa ngumi ambazo zimejaa mbinu za kiufundi kama walivyo mabondia wengine.

Kuelekea katika pambano hilo, Watanzania wengi waliona ni kama Hamadi Furahisha ‘Mfupa wa Sokwe’, ameonewa au kupewa mzigo mzito wa kupigana na Phiri kwenye pambano la Boxing on Boxing Day ambalo limefanyika Disemba 26, mwaka huu kwa kutegemea asingweza kufika popote kama ilivyo kwa mabondia wengine wa Tanzania waliowahi kupigana na bondia huyo.

Phiri mara ya kwanza kuja Tanzania ilikuwa ni mwaka 2020 katika pambano ambalo lilifanyika mkoani Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri katika pambano ambalo lilikuwa gumu kwa Cheka licha ya kufanya vizuri katika raundi saba za awali huku Phiri akifanikiwa kufanya vyema kwenye raundi nne za mwisho.

Matokeo yakampa Cheka ushindi wa pointi katika pambano la raundi 12 lakini likaibuka kundi la mashabiki wengi wakidai Cheka alipigwa na Phiri  lakini wakasahau kuwa Cheka alichukua raundi saba za awali kabla ya kukata upepo uliopelekea mpinzani wake kufanya vizuri kwenye raundi nne za mwisho.

Kutokea hapo jina la Phiri lilianza kuimbwa na mashabiki wengi kabla ya mwaka 2021 ambapo safari hii kibarua alipewa Mtanzania Yonas Segu kutetea mkanda wake wa ubingwa wa WBF Afrika kwenye uzani wa Light katika pambano ambalo lilifanyika Ubungo Plaza.

Licha ya ufundi wa Segu lakini alijikuta akiishia raundi ya tisa baada ya kukubali kichapo cha Technical Knockout na akapoteza mkanda wake wa ubigwa, jina la Phiri ndiyo likazidi kupanda thamani nchini.

Kutokana na hivyo Oktoba mwaka 2021 akarudishwa tena nchini lakini kazi akapewa Salmini Mtango kutoka Tanga ambaye aliaminika angweza kumaliza ubishi wa Phiri matokeo yake Mtango akaponea chupuchupu katika pambano ambalo lilimizika kwa sare.

Mwaka 2023, Mtanzania mwengine, Adam Lazaro akamtaka Phiri ambapo Lazaro alijikuta akiishia raundi ya nne katika pambano la raundi kumi ambalo lilifanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani kwa kukubali kichapo cha Knockout baada ya hapo hakuna bondia Watanzania aliyetaka kumsikia Phiri.

Mwaka huu, Hamadi Furahisha akaomba aletewe kwenye pambano ambalo limeigwa wikiendi iliopita na akaweza kuwaonyesha Watanzania ngumi za kisasa zinavyokuwa.

Furahisha mwenye rekodi ya kucheza jumla ya mapambano 16 akiwa ameshinda 12 kati ya hayo Knockout ikiwa moja, amepigwa mara mbili kati hizo moja akipigwa kwa Knockout na ametoka sare mara mbili.

Wakati Phiri yeye akiwa na rekodi ya kucheza mapambano 16, akiwa ameshinda mara tisa kati ya hizo nane akiwa ameshinda Knockout na amepigwa mara tano kati ya hizo tatu ikiwa ni Knockout na ametoka sare mara mbili.

Katika pambano hilo ambalo ndiyo liliwavutia mashabiki wengi kutokana na mchezo wa mzuri wa Furahisha kwa kuweza kumdhibiti katika raundi zote kumi za pambano hilo kwa kuweza kumpiga kwa hesabu kali kiasi cha kumfanya Phiri akose kujitetea.

Furahisha amefanikiwa kumpiga na kumfundisha namna ngumi zinavyochezwa huku pambano lake litakwa kuwa bora  na lilipaswa kuwa pambano kuu tofauti na alilocheza Hassan Mwakinyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *