BAADA ya Mwanaspoti kuripoti taarifa kwamba mshambuliaji Abdallah Idd ‘Pina’ alikuwa ameachana na Pamba Jiji aliyoitumikia kwa miezi sita na kurejesha majeshi yake Zanzibar kujiunga na Muembe Makumbi, nyota huyo ameanika kilichosababisha yeye kurudi visiwani humo.

Pina alirejea uwanjani baada ya kuwa majeruhi wa muda mrefu, amesema ni kweli amerudi visiwani Zanzibar kujiunga kwa mkopo na Muembe Makumbi inayoshiriki Ligi Kuu ya visiwani humo (ZPL) kwa ajili ya kujitafuta baada ya kukaa nje kwa muda akiuguza jeraha la goti.

Nyota huyo aliyekuwa mfungaji bora msimu uliopita akiwa na Mlandege akifunga mabao 21 na asisti 12 kupitia mechi 22, aliliambia Mwanaspoti amefurahishwa kupewa nafasi hiyo kwani anaamini ligi atakayocheza haina presha kubwa kama ilivyo Ligi Kuu Bara.

Pina aliyejiunga na Pamba Jiji kwa mkataba wa miaka miwili alikanusha pia taarifa za kuvunjiwa mkataba akiweka wazi, anaenda kwa mkopo Muembe Makumbi ili kurudisha utimamu aliokuwa nao baada ya kukaa kwa nje muda mrefu.

“Yanazungumzwa mengi ukweli, ila ukweli ni kwamba naenda Muembe Makumbi kwa mkopo wa miezi sita ili kutafuta utimamu wa mwili baada ya kukaa nje kwa muda mrefu, kwani tangu nimejiunga na Pamba Jiji sijapata nafasi ya kucheza mechi nyingi niliumia goti,” amesema Pina kuongeza;

“Nimeuomba uongozi unitoe kwa mkopo huku ambapo ligi yake haina presha tayari nimeanza mazoezi na timu na inatarajia kushiriki mechi za Kombe la Mapinduzi 2026, naamini nikianzia huku na kucheza ligi utimamu wangu na ubora ukirudi nitarudi kumalizia mkataba wangu Pamba.”

Pina amesema Ligi Kuu ya Zanzibar haina presha kubwa kama ilivyo ya Bara, hivyo anaamini ndani ya miezi sita ataweza kurudi kwenye ushindani na kurudisha ubora aliomaliza nao akiwa Mlandege.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *