Kamati hiyo imepitisha rasimu ya azimio A/C.5/80/L.6 kuhusu bajeti ya mpango ya 2026, ambayo imegawanywa katika sehemu tatu: mgao wa bajeti kwa mwaka huo, makadirio yaliyorekebishwa ya mapato, na mipango ya kufadhili matumizi yaliyoidhinishwa.

Licha ya kile wajumbe walichokitaja kuwa mchakato mgumu na wa haraka wa majadiliano, matokeo hayo yamekaribishwa kwa upana kama ishara ya ushirikiano na maridhiano kati ya makundi ya kikanda na kisiasa.

Muungano wa Ulaya wasifu mafanikio ya mageuzi

Muungano wa Ulaya umesifu kupitishwa kwa bajeti hiyo na hatua zilizopigwa katika kuweka mfumo mpya wa mishahara na viwango vya ajira kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, ukieleza kuwa ni mojawapo ya matokeo yenye matarajio makubwa zaidi yaliyopatikana kupitia mazungumzo katika miaka ya karibuni.

“Tumeafikiana kuhusu moja ya matokeo yenye dhamira kubwa zaidi katika mfumo wa pamoja wa Umoja wa Mataifa,” amesema mwakilishi wa Muungano wa Ulaya, akizungumza kama mwangalizi. Amebainisha kuwa wajumbe walipitia “mazungumzo magumu, yasiyo na ufanisi na yanayochosha,” lakini hatimaye walionesha uwajibikaji na ushirikiano.

Muungano wa Ulaya pia umetaja kikao hicho kuwa hatua muhimu katika utekelezaji wa Mpango wa UN80, unaolenga kuuboresha na kuufanya Umoja wa Mataifa uwe na ufanisi zaidi. Ingawa umeunga mkono kikamilifu ajenda ya mageuzi, Muungano wa Ulaya umeonya kuwa athari zake kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa lazima zisimamiwe kwa uangalifu.

Kundi la Afrika lapongeza matokeo yaliyo na uwiano

Mwakilishi wa Angola, akizungumza kwa niaba ya Kundi la Afrika, amesema kikao hicho kimefanyika chini ya “mazingira ya kipekee” kutokana na ratiba fupi ya mazungumzo, lakini Kamati imeweza kufanikisha matokeo chanya.

Amesema roho ya ushirika na maridhiano imewezesha kufikiwa kwa makubaliano kuhusu masuala muhimu ya bajeti na kulinda tabia ya Kamati kama chombo cha kiserikali kinachoongozwa na uanachama. Kundi la Afrika pia limepongeza kupitishwa, kwa mwaka wa pili mfululizo, kwa azimio kuhusu Ujumbe maalum wa kisiasa, likihakikisha usimamizi na uangalizi wa kiserikali kwa Ujumbe huo, zikiwemo zile zinazofanyika barani Afrika.

China yataka kupunguza gharama na kuongeza uwazi

China imetoa wito wa utekelezaji kamili wa mageuzi yanayolenga kupunguza gharama za Umoja wa Mataifa na kuboresha ufanisi, ikisisitiza kuondolewa kwa urudufu wa majukumu na kupunguza urasimu.

China imesisitiza kuwa Nchi Wanachama lazima ziwe na nafasi kuu katika mchakato wa mageuzi, huku Sekretarieti ikitoa ushauri na mapendekezo kwa uwazi. Pia imesisitiza umuhimu wa kuimarisha ufanisi na uwazi wa mipango ya programu katika Kamati Kuu za Umoja wa Mataifa.

Marekani yaangazia akiba na upunguzaji wa wafanyakazi

Marekani imesifu kile ilichokiita “mageuzi ya busara,” ikiipongeza Kamati ya Tano kwa kupitisha bajeti nyepesi na yenye vipaumbele vilivyobainishwa vizuri zaidi.

Kwa mujibu wa ujumbe wa Marekani, bajeti ya 2026 inaonesha akiba ya dola milioni 57 ikilinganishwa na mwaka uliopita, na inajumuisha kufutwa kwa karibu nafasi 2,600 za ajira, hatua iliyosemwa kusaidia kupunguza urasimu na kurejesha mkazo kwenye vipaumbele vya msingi. Marekani imesisitiza kuwa mageuzi si zoezi la mara moja, bali ni mchakato unaoendelea, huku ikitarajia ufanisi zaidi katika bajeti zijazo.

Brazil yaonya kuhusu kuchelewa kwa michango

Brazil imeunga mkono kupitishwa kwa bajeti hiyo lakini ikatoa onyo kuhusu tatizo la kucheleweshwa kwa malipo ya michango ya lazima, hasa kutoka kwa wachangiaji wakubwa.

“Michango lazima ilipwe kwa wakati, kwa ukamilifu na bila masharti,” amesema mwakilishi wa Brazil, akionya kuwa madeni sugu yanadhoofisha uwezo wa kupanga na utekelezaji wa maagizo ya Umoja wa Mataifa. Ameongeza kuwa mageuzi yanapaswa kuwa yenye uwiano na kuzingatia mahitaji ya watu, bila kusahau wale wanaotegemea zaidi Umoja wa Mataifa, wakiwemo waathirika wa migogoro, njaa na maendeleo duni.

Mdhibiti wa UN aeleza mzigo kwa Sekretarieti

Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Umoja wa Mataifa, Chandramouli Ramanathan, ameeleza shinikizo kubwa lililokuwepo katika kuandaa bajeti ya 2026, akisema iliandaliwa ndani ya kipindi cha chini ya wiki sita na ikajumuisha jedwali 345 za bajeti.

Amesema Sekretarieti ilijibu zaidi ya maswali 2,000 kutoka Kamati ya Ushauri ya Masuala ya Utawala na Bajeti (ACABQ) na sasa inakabiliwa na changamoto ya haraka ya kufutwa kwa nafasi 2,900 za ajira.

Kuhakikisha wafanyakazi walioathiriwa wanalipwa na kuungwa mkono ipasavyo wakati wa mpito, amesema, kutakuwa jukumu muhimu Umoja wa Mataifa unapoanza mwaka mpya.

Kupitishwa kwa bajeti ya 2026 kunaweka msingi wa mjadala zaidi kuhusu mageuzi, ufanisi na ufadhili wa Umoja wa Mataifa, wakati Nchi Wanachama zinaendelea kutafuta njia bora za kuiwezesha taasisi hiyo kukabiliana na changamoto za dunia huku ikisimamia rasilimali chache.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *