Arusha. Mahakama ya Rufaa ya Tanzania imebatilisha hukumu ya kifungo cha miaka 20 jela na faini ya zaidi ya Sh343.8 milioni aliyokuwa amehukumiwa raia wa Nigeria, Okwudili Nnaman Agu, kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini.

Agu alikuwa alitiwa hatiani baada ya kukiri kosa la kusafirisha heroini yenye uzito wa gramu 1,273.69, yenye thamani ya zaidi ya Sh114.6 milioni, ambapo alikamatwa Desemba 29, 2013 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.

Awali alivyofikishwa mahakamani wakati wa usikilizwaji wa awali alikana kosa ila baadaye kesi hiyo ilipoendelea kusikilizwa miaka miwili baadaye alikiri kosa na kuhukumiwa adhabu hiyo.

Mrufani huyo alitaka rufaa Mahakama ya Rufaa akipinga hukumu hiyo na kudai kuwa alikiri kosa kwa kutoelewa makosa, kwani kipindi chote cha kesi alikana kutenda kosa hilo.

Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa ambao ni Ferdinand Wambali, Lucia Kairo na Deo Nangela,walitoa hukumu hiyo Desemba 29,2025 na nakala yake kuwekwa kwenye tovuti ya mahakama.

Jopo la majaji hao limebaini kuwa kukiri kosa kwa mshtakiwa hakukufanywa kwa kufuata taratibu za kisheria, hivyo hukumu hiyo haikuwa sawa kisheria.

Katika hukumu yao iliyotolewa Desemba 29, 2025, majaji hao wamesema Mahakama Kuu ilifanya makosa kumtia hatiani Agu kwa kukiri kosa ilhali ukweli wa kesi haukuwekwa wazi wala kurekodiwa ipasavyo, kama inavyotakiwa kisheria.

Jaji Wambali amesema Mahakama hiyo imebaini kuwa kukiri kosa kwa mshtakiwa hakukuwa wazi wala bila shaka kama inavyotakiwa kisheria na kuwa Mahakama Kuu ilifanya makosa kumtia hatiani mshtakiwa kwa kukiri kosa, ilhali taratibu za kisheria za kuthibitisha kukiri huko hazikuzingatiwa.

Mahakama hiyo imebatilisha hukumu iliyotolewa Novemba 26, 2021, imefuta hatia na kuweka kando adhabu ya kifungo na faini aliyokuwa amepewa Agu.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufaa haikumwachia huru mshtakiwa huyo, badala yake imeamuru kesi hiyo irudishwe Mahakama Kuu kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kuanzia hatua ilipofikia Juni 19, 2019, ambapo mashahidi watatu wa upande wa Jamhuri walikuwa tayari wameshatoa ushahidi na kuwa mrufani huyo  ataendelea kushikiliwa mahabusu akisubiri kuendelea kwa kesi yake Mahakama Kuu.

Ilivyokuwa

Awali Mahakama Kuu ilimtia hatiani mrufani kwa kosa la usafirishaji haramu wa dawa za kulevya kinyume na kifungu cha 16(b) cha Sheria ya Dawa za Kulevya na Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Dawa za Kulevya, Sura ya 95.

Awali, baada ya mrufani kufikishwa mahakamani kwa ajili ya kesi katika Mahakama Kuu kwa ajili ya usikilizwaji wa awali alikana kosa ambapo kesi hiyo ilisikilizwa hadi Juni 19,2019 kabla ya kuahirishwa ambapo mashahidi watatu wa upande wa mashtaka walishatoa ushahidi wao pamoja na vielelezo vitano.

Kulingana na rekodi ya rufaa, kesi hiyo iliendelea tena Novemba 26, 2021 baada ya zaidi ya miaka miwili ambapo siku hiyo alikiri hatia kuhusu kosa hilo.

Jaji Wambali amesema kuwa awali rufaa hiyo iliahirishwa kusikilizwa kwa sababu mrufani alionyesha nia yake ya kutafuta wakili ili amtetee ambapo baadaye wakati wa usikilizwaji alisitisha nia hiyo na kuomba Mahakama ikubali rufaa yake na kumwachia huru.

Alidai kwamba alikiri kosa kwa sababu ya kutoelewa na makosa kwani katika kipindi chote cha kesi alikuwa ameshikilia kukiri kutokuwa na hatia.

Sababu nyingine ya rufaa ni kwamba rekodi ya kesi ya tarehe hiyo inaonyesha wazi kwamba alikiri kosa mara mbili huku maneno ambayo anachukuliwa kuwa amesema ni tofauti. Katika uwasilishaji wake, kwanza, anarekodiwa akisema; “ni kweli. Ninakiri kosa”. Pili, amesema kwamba; “Bwana wangu ninakiri kosa kwa shtaka. Ni wakati”.

Mrufani huyo amedai mbali na kurekodiwa kwamba alikiri kosa mara mbili kuliwasilishwa na mahakama ya mwanzo, haijulikani ni kwa nini maneno anayodaiwa kusema wakati wa maombi hayo yanatofautiana, na kuwa jaji alihitimisha kimakosa kwamba ombi lake ni kinyume kabisa na mwongozo uliowekwa ambao lazima uzingatiwe katika kufikia uamuzi kama huo.

Ili kuunga mkono msimamo wake kuhusu mazingira ambayo madai ya kukiri kosa yanaweza kupingwa, alirejelea maamuzi katika kesi ya Laurent Mpinga dhidi ya Jamhuri [1983] T.L.R. 166, Kalos Punda dhidi ya Jamhuri, Rufaa ya Jinai Nambari 153 ya 2005 (haijaripotiwa), Safari Deemay dhidi ya Jamhuri, Rufaa ya Jinai namba 269 ya 2011.

Sababu nyingine alidai kwamba rekodi ya kesi inaonyesha tu kwamba ukweli ulioandikwa ulisomwa kwake, hata hivyo, ukweli huo hauonekani katika rekodi ya rufaa na rekodi ya kesi inaonyesha kwamba ni baadhi tu ya vielelezo vilivyowasilishwa tarehe hiyo, huku vingine vikiwasilishwa wakati wa kesi.

Katika suala hili, mrufani amesema kwamba kukiri ukweli wote kulijumuisha vielelezo vitano vinavyodaiwa vilivyowasilishwa wakati wa kesi lakini hakusomewa, na kueleza kuwa kwa kuzingatia makosa hayo haijulikani ni ukweli gani alikiri kuwa sahihi na wa kweli kinyume na uamuzi wa mahakama ya mwanzo.

Kwa upande wa mjibu rufaa, aliunga mkono rufaa hiyo na kueleza kuwa bila ya kuwepo kwa ukweli ambao ulirekodiwa kuwa umesomwa, haiwezi kuhitimishwa kwamba mrufani alikiri ipasavyo kwamba ukweli na vielelezo vilikuwa sahihi na vya kweli.

Wakili wa mjibu rufaa alikubaliana na mawasilisho ya mrufani na akaiomba Mahakama iruhusu rufaa hiyo kufuta hatia, na kuomba badala ya kumwachia mrufani kama alivyoomba, aliomba Mahakama iwasilishe jalada hilo Mahakama Kuu kwa ajili ya kuendelea na kesi hiyo kutoka pale ilipoishia kabla ya kuharibika.

Uamuzi Majaji

Jaji amesema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, wanaona ni muhimu kupitia mwenendo ikiwemo wa Novemba 26,2021 ambao unaonyesha kuwa mshtakiwa alikumbushwa kuhusu shtaka dhidi yake ambapo alikiri hatia na kutiwa hatiani.

Jaji Wambali amesema kuwa imeamuliwa kwamba kabla ya Mahakama kumtia hatiani mshtakiwa kwa kukiri hatia, ni lazima iridhike bila shaka kwamba, ukweli uliotolewa na upande wa mashtaka unathibitisha au kufichua vipengele muhimu vya kosa ambalo ameitwa kukiri na amekiri kweli.

Amesema muhimu zaidi, Mahakama imeweka vigezo ambavyo vinaweza kuzingatiwa kabla ya kuhitimisha kwamba hoja ya mshtakiwa haina shaka ambapo imewekwa misingi kadhaa, ikiwemo mtu anaposhtakiwa, shtaka na maelezo yote yanapaswa kusomwa kwake, kadri iwezekanavyo katika lugha yake mwenyewe, lakini ikiwa hilo haliwezekani basi kwa lugha ambayo anaweza kuzungumza na kuelewa.

Aidha anapaswa kuelezwa vipengele vyote muhimu vya kosa linaloshtakiwa na ikiwa mshtakiwa anakubali vipengele hivyo vyote muhimu, inapaswa kurekodiwa kile mshtakiwa amesema, na kisha kukiri rasmi hatia.

Jaji amesema baada ya kupitia wameona haijulikani ni kwa nini mrufani aliitwa kukiri mara mbili na, katika matukio yote mawili, inadaiwa alikiri bila shaka hatia ingawa taarifa iliyorekodiwa kuhusu ombi lake ilitofautiana.

Baada ya kupitia hoja zote majaji hao walibatilisha kesi ya Novemba,26 2021, kufuta hatia na kuweka kando hukumu iliyotolewa kwa mrufani na kuamuru jalada lirejeshwe Mahakama Kuu kwa ajili ya kuendelea na kesi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *