Ufaransa itachunguza katika mwezi huu wa Januari muswada unaokusudia kupiga marufuku matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka 15 na uchukuaji wa simu za mkononi katika skuli za sekondari.

Kwa mujibu wa mtangazaji wa Franceinfo, Baraza la Nchi la Ufaransa litachunguza muswada huo Januari 8 kwa lengo la kupiga marufuku utumiaji wa mitandao ya kijamii kwa vijana wadogo walio na umri wa chini ya miaka 15 na kupiga marufuku pia matumizi ya simu za mkononi katika skuli za sekondari kuanzia mwaka mpya wa masomo ambao ni Septemba 2026.

Kwa mujibu wa duru za serikali, muswada huo umeandaliwa kwa namna ambayo utahakikisha unaendana na sheria za Ulaya, kinyume na uliotangulia ambao haukufanikiwa.

Mnamo mwezi Novemba, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema anataka kupanua wigo wa marufuku ya matumizi ya simu za mkononi kwa skuli za sekondari kuanzia mwanzo wa mwaka wa masomo wa 2026-2027 na kuweka marufuku ya mitandao ya kijamii kwa vijana walio na umri chini ya miaka 15 au 16.

Marufuku ya simu za mkononi tayari imekuwepo kuanzia skuli za maandalizi hadi za kati chini ya sheria ya mwaka 2018, japokuwa wakati mwingine imeonekana kuwa na ugumu wa kutekelezwa.

Tafiti nyingi za kiakademia zimeorodhesha hatari za afya ya akili za matumizi ya mitandao ya kijamii kwa vijana wadogo pamoja na hatari za kuvurugwa na simu za mkononi kwa vijana mabarobaro.

Itakumbukwa kuwa mwishoni mwa mwezi Novemba, Australia ilipitisha sheria za kupiga marufuku watoto na vijana wadogo kutumia mitandao ya kijamii, ukiwa ni uamuzi wa kwanza wa aina yake kuchukuliwa na serikali yoyote duniani.

Katika taarifa aliyotoa Novemba 21, Waziri Mkuu wa Australia Albanese alieleza kwamba, mitandao ya kijamii inasababisha madhara ya kijami na akafafanua kwa kusema: “tunataka watoto wa Australia wauishi utoto wao, na tunataka wazazi wajue kuwa Serikali iko upande wao. Haya ni mageuzi ya kihistoria. Tunajua baadhi ya watoto watatafuta mbinu nyingine, lakini tunatuma ujumbe kwa makampuni ya mitandao ya kijamii yaweke sawa utendaji wao”…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *