
Rabat, Morocco. Kipa, Luca Zidane anaendelea kuwa gumzo na chaguo pendwa kwa timu ya taifa ya Algeria, wakati taifa hilo jana lilikuwa dimbani kusaka clean sheet ya tatu ya hatua ya makundi dhidi ya Guinea ya Ikweta katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCION) 2025.
Mabingwa hao mara mbili wa Afrika walianza kampeni ya fainali hizo za 35 zinazofanyika Morocco kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Sudan, kisha wakaichapa Burkina Faso kwa bao 1-0 matokeo yaliyowahakikishia nafasi ya kwanza katika Kundi E. Katika mechi hizo, Zidane alifanya sevu muhimu zilizoisaidia timu ya kocha Vladimir Petkovic kubaki salama.
Katika mechi sita za awali kabla ya mashindano haya, Algeria mara moja tu ilikomaa na kutoruhusu bao (clean sheet) na ikumbukwe iliondolewa katika hatua ya makundi mwaka 2021 na 2023 baada ya kutwaa ubingwa wa Afrika 2019 pale Misri kwa kuichapa Senegal ambayo awali zilikuwa katika kundi moja pamoja na Tanzania na Kenya.
Hata hivyo, tangu Luca Zidane, mwana wa gwiji wa soka wa Ufaransa na bingwa wa Kombe la Dunia, Zinedine Zidane, alipobadilisha uraia wa kimichezo na kuanza kuichezea Algeria Septemba mwaka jana baada ya awali kuchezea Ufaransa katika soka la vijana, Algeria imefanikiwa kupata clean sheet mbili katika michezo mitatu aliyocheza katika mashindano yote.
Kipa huyo mwenye umri wa miaka 27 anayechezea Granada, amezoea haraka majukumu yake tangu alipochaguliwa kuwa kipa namba moja, alisema kocha Petkovic.
“Zidane amechangia kwa kiasi kikubwa ushindi katika mechi zote mbili. Ameanza kuzoea timu na kupata uzoefu kwa muda mfupi sana,” alisema kocha huyo juzi Jumanne timu ikijiandaa na mechi ya jana Jumatano.
Licha ya kujiunga na timu tangu Oktoba mwaka jana, Zidane hajasita kuwaongoza na kuwaelekeza wachezaji wenzake uwanjani, kwa mujibu wa beki Rayan Ait Nouri.
“Luca ni mtu mzuri sana. Amezoeana haraka na kikosi, anazungumza sana uwanjani na anatupa msaada mkubwa. Ni mchezaji na mtu anayefaa kabisa ndani ya timu,” aliongeza Ait Nouri.
Algeria ilitarajiwa kupata clean sheet nyingine dhidi ya Guinea ya Ikweta katika mechi ya mwisho kutokana na ukweli timu hiyo tayari imeshaondolewa michuanoni baada ya kufunga bao moja tu katika michezo miwili iliyopita, huku mabingwa wa 2019 wakionekana kuwa moto katika kundi E tangu mwanzo wa michuano hiyo.