Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kuhimiza kuanzishwa na kuendelezwa kwa mabonanza, ligi na matukio ya michezo yenye hadhi ya kitaifa na kimataifa ili Zanzibar iwe kituo muhimu cha utalii wa michezo katika ukanda huo.   

Kauli hiyo ameitoa leo Januari Mosi, 2026 katika bonanza la mazoezi ya viungo kitaifa liloambatana na matembezi kutoka Kisonge hadi Viwanja vya New Amaan Complex.

Amesema michezo ni sekta yenye mchango mkubwa katika kuimarisha utalii na uchumi wa nchi kwani kupitia mashindano ya michezo ya kimataifa Zanzibar inaweza kuvutia watalii, wawekezaji na wageni kutoka mataifa mbalimbali na kuongeza pato la taifa na kuimarisha ajira kwa vijana.

“Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi na wadau wa michezo katika kuhakikisha miundombinu ya michezo inaendelezwa ili kukidhi viwango vya kimataifa na kuitangaza Zanzibar kama kitovu cha utalii wa michezo,” amesema.

Amesema malengo ya Serikali ni kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya michezo kuanzia ngazi ya chini hadi juu ili kuwaandaa vijana kuwa wanamichezo wa kulipwa na wenye ushindani kimataifa.

Alibainisha kuwa kupitia programu madhubuti za mafunzo, nidhamu na usimamizi bora wa michezo ana imani kuwa Zanzibar itaendelea kutoa wanamichezo watakaouza vipaji vyao katika ligi na vilabu vya mataifa mengine na kuinua hadhi ya taifa lao pamoja na kuboresha maisha ya wanamichezo na familia zao.

Dk Mwinyi amesema Serikali imeimarisha kwa kiwango kikubwa sekta ya michezo kutokana na ujenzi wa miundombinu yenye viwango vya kimataifa ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa Amaan Complex, Gombani Pemba na Uwanja wa Mau.

Amesema ujenzi unaendelea kwa viwanja vingine 17 katika wilaya na mikoa yote nchini ambapo baadhi vimeshakamilika na vitaendelea kufunguliwa katika maadhimisho ya sherehe za miaka 62 ya Mapinduzi.

Ametumia fursa hiyo kuiagiza Wizara ya Habari Sanaa Utamaduni na Michezo kuhakikisha inaweka usimamizi na utunzaji mzuri wa viwanja hivyo na kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kuvitumia kama ilivyokusudiwa.

Akizungumzia mazoezi ya viungo amesema ni jambo muhimu katika maisha ya mwanaadamu kwani yanachangia katika kuimarisha afya ya mwili na akili na kukinga magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, bonanza hilo ni jukwaa muhimu la kuwakumbusha kuwa afya njema ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Kupitia mabonanza haya ya mazoezi tunajenga na kuimarisha udugu, urafiki na mshikamano wa kitaifa,” alisema.

Rais Mwinyi alitoa msisitizo maalumu juu ya umuhimu wa kushiriki na kuendeleza michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu mpira wa kikapu, wavu, riadha, michezo ya majini pamoja na michezo ya asili.

Naye Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Dk Riziki Pembe Juma, amempongeza Rais Mwinyi  kuungana na wana mazoezi katika kudumisha afya zao kwani afya ya mtu ni jukumu lake hivyo ni vyema kila mmoja kuhakikisha ana kila sababu ya kulinda afya yake kwa nguvu zake zote.

Katibu wa Wizara hiyo, Mattar Zahor amesema wanajivunia mafanikio makubwa kwani bonanza hilo limeshirikisha zaidi ya vilabu vya mazoezi 165 ambapo 100 kutoka Unguja, 25 kutoka Pemba na vilabu 40 kutoka Tanzania bara pamoja na washiriki zaidi ya 500 wakiwemo wananchi wa rika mbalimbali.

Amesema hiyo ni ishara tosha na jamii kuwa na muamko wa kushiriki michezo na kuzingatia afya zao sambamba na kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza sekta hiyo nchini.

Kwasasa Zanzibar ina vyama 47 vya michezo vikiwemo vya michezo ya asili kama bao na karata jambo linaloonesha dhamira ya Serikali  ya awamu ya nane ya kulinda, kuendeleza na kuenzi michezo ya kisasa na ile ya asili kama sehemu ya utamaduni wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *