
Mbeya. Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda amewaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali na kudumisha amani, akisema utekelezaji wa miradi miwili ya kimkakati katika wilaya hiyo utakuwa sehemu ya historia endapo itakamilika kwa wakati.
Kauli hiyo ameitoa usiku wa mkesha wa kuukaribisha Mwaka Mpya wa 2026, Desemba 31, katika viwanja vya Uhindini jijini Mbeya, wakati Watanzania na wananchi wa mataifa mbalimbali duniani walipokuwa wakiuaga Mwaka 2025 na kuukaribisha mwaka mpya 2026, kila mmoja akiwa na kumbukumbu na historia yake.
Akizungumza katika mkesha huo, Itunda amesisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kushirikiana na Serikali pamoja na viongozi kwenye ngazi zote huku wakidumisha amani, upendo na mshikamano kama msingi wa maendeleo.
“Tunapouendea Mwaka Mpya wa 2026, tuendelee kufanya kazi kwa bidii, tudumishe amani, upendo na mshikamano na tushirikiane na Serikali kusaka maendeleo ya kweli,” amesema Itunda.
Amesema kwa Wilaya ya Mbeya, Serikali imeonesha ushirikiano mkubwa katika utekelezaji wa miradi miwili ya kimkakati, ukiwamo ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Igawa hadi Tunduma pamoja na Mradi wa Maji kutoka Mto Kiwira, akibainisha kuwa miradi hiyo ina mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake, mmoja wa wananchi walioshiriki mkesha huo ulioandaliwa na Mbunge wa Mbeya Mjini, Patrick Mwalunenge, Charles Martin amesema mwaka 2025 ulikuwa na matukio mchanganyiko ya furaha na changamoto.
Amesema 2025 kwa upande wake ulikuwa wa mafanikio kwa kufanikisha mipango yake, ingawa tukio la Oktoba 29 litaendelea kubaki katika kumbukumbu za wengi kutokana na kilichotokea.
“Kwa mwenye uelewa, huwezi kumhadithia kuhusu Oktoba 29, binafsi namshukuru Mungu nimefanikiwa kuumaliza salama Mwaka 2025 nikiwa na familia yangu na nawatakia mafanikio wengine katika Mwaka Mpya wa 2026,” amesema Martin.
Ameishauri Serikali kuendelea kuwasikiliza wananchi kama inavyoonekana sasa, akitolea mfano namna mawaziri na wabunge wanavyowafikia wananchi, akiwemo Mbunge wa Mbeya Mjini.
Naye Mbunge wa Mbeya Mjini, Patrick Mwalunenge amewashukuru wananchi kwa ushiriki wao na kuwaomba kuendelea kushirikiana na Serikali, akisisitiza kuwa itaendelea kutimiza wajibu wake wa kuwaletea maendeleo.
“Huu ni mwanzo. Niwaombe tuendelee kufanya kazi kwa maslahi ya Mbeya Mjini na Taifa kwa ujumla. Serikali iko bega kwa bega na wananchi katika kuwaletea maendeleo,” amesema Mwalunenge.