Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amesema bado anaendelea kukataa matukio ya utekaji kwa kuwa hayampendezi Mungu, kinyume cha sheria za nchi na hata dini haziyataki.

Kauli hiyo ya Askofu Gwajima ni ya kwanza anaitoa akiwa katika kanisa hilo, tangu alipohubiri Juni 2, 2025 na kanisa lake kufungiwa kwa kile kilichoelezwa linaingiza masuala ya siasa, jambo lililotajwa kuwa kinyume cha sheria za usajili wake.

Katika mahubiri hayo ya Juni 2, kiongozi huyo wa kiroho alitangaza maombi ya mfungo wa kuombea kukoma kwa matukio ya utekaji nchini na baadaye Novemba 24, 2025 Jeshi la Polisi lilitangaza kumsaka.

Hata hivyo, ilipofika Novemba 30, 2025 Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alitangaza Askofu Gwajima aache kusakwa na polisi ili aungane na wengine katika juhudi za kuleta mshikamano na umoja wa Taifa.

Askofu Gwajima ametoa kauli hiyo usiku wa kuamkia leo, Alhamisi Januari 1, 2026 katika mahubiri yake ya kuukaribisha mwaka mpya mbele ya umati wa waumini waliojaa kanisani hapo na kushangilia kila alipoweka kituo wakati wa kuhubiri.

Ameianza hoja hiyo kwa kuwaambia waumini wake kuwa, magumu waliyoyapata ni kwa sababu yeye alikataa utekaji na kwamba hadi sasa anakataa utekaji.

“Unajua magumu uliyoyapata ni kwa sababu mimi nilikataa utekaji, mpaka leo nakataa vile vile. Ndio wewe ikaingia kwenye magumu hayo,” amesema.

Amesema amekataa matendo hayo kwa sababu Mungu hataki, sheria ya nchi haitaki, dini hazitaki yeye, waumini wake na nchi yote haitaki matendo hayo.

Amesema kama kusudi uliloitiwa binadamu halijaisha, haijalishi kuna simba kiasi gani hawatakudhuru, kwani Mungu ameweka kusudi kwa kila aliyemuumba.

“Mungu ameweka kusudi ndani yako, ikiwa halijaisha hakuna wa kukuua duniani na usifikirie Mungu ameweka makusudi juu ya walokole pekee hapana, juu ya binadamu wote,” amesema.

Ameeleza Mungu ameweka sababu ya kuumbwa kwa kila binadamu na isipotimia maana yake ameshindwa yeye, hivyo hawezi kukubali kushindwa.

Askofu Gwajima amesema kwa mambo yanayomhusu Mungu atarudi kwa Mungu hata akiwa mzee bila kubadilika, kujadiliana kwani nyakati zinazoendewa hazipaswi kupoa.

“Ukienda kwenye kanisa lolote ukiona kama kuna michanganyochanganyo ondoka hapo hata kama ni Ufufuo na Uzima.

“Maaskofu wetu wawili hawapo Dickson na Mwanamapinduzi walipigana hadi wakakimbia nje ya nchi kuokoa uhai na leo tutawaombea. Yeyote asiye mpiganaji si mwanangu,” amesema.

Ameyagawanya mahubiri hayo katika shukurani tatu, kwanza ni kufanya ibada ya mkesha wa mwaka mpya wakiwa katika kanisa ambalo limeezekwa na wenyewe.

Ameeleza shukurani ya pili ni kuuvuka mwaka 2025 aliouita wa malango yaliyoinuka ili wafalme waingie.

Shukurani ya tatu, amesema ni kupita katika mitihani na hatimaye watu wameshinda katika mitihani hiyo, ingawa hakuifafanua kwa kina.

Kwa kuwa Mungu amewapa ushindi, amesema ni uthibitisho kwamba wao ni wapiganaji wasio wa kawaida.

Amesema kanisa lisilojua vita sio la Yesu kwani uhalisia wa Kanisa limezaliwa msalabani wakati mwanzilishi wake amevaa taji la miba.

Amewafananisha waumini wa kanisa lake na majasusi wa mbinguni waliounda timu moja yakiwa na ajenda na yamepewa nguvu na hayatakufa leo wala kesho.

Amesema walimfurahisha walipokuwa wakihama ukumbi kwa ukumbi, akisema alijiuliza watu hao walijuaje.

“Kanisa la Yesu siyo lile unachapwa kushoto unatega na kulia, kabisa la Yesu ni lile linachapwa kushoto unachapwa zaidi,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *