Ofisi Kuu ya Takwimu ya Palestina imeripoti kuwa mwaka 2025 ulikuwa mwaka mbaya zaidi katika uga wa kibinadamu na idadi ya jamii ya watu huko Palstina kutokana na vita vya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na kuongezeka kwa ukiukaji wa sheria katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, ikiwa ni pamoja na Quds Mashariki.

Ofisi Kuu ya Takwimu ya Palestina imesema katika ripoti yake ya kufunga mwaka wa 2025 kwamba mauaji ya kimbari, watu kulazimishwa kuhama makazi yao, na uharibifu mkubwa wa miundombinu muhimu, yote haya yamesababisha maafa makubwa na ya muda mrefu kwa utulivu wa kijamii, hali ya kiuchumi na kijamii na haki za binadamu katika ardhi za Palestina.

Ofisi Kuu ya Takwimu ya Palestina imeinukuu Wizara ya Afya ya Palestina na kuripoti kuwa, Wapalestina zaidi ya 72,000 wameuawa shahidi tangu kuanza vita na mauaji ya kimbari ya Israel Oktoba 7, 2023 ambapo asilimia 98 ya vifo vimesajiliwa huko Gaza. Kiwango hicho kimetajwa kuwa kikubwa sana kuwahi kushuhudiwa katika historia ya mashambulizi ya Israel dhidi ya Wapalestina. 

Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Disemba 2025, wahanga hao ni pamoja na watoto 18,592 na wanawake wapatao 12,400, huku takriban watu 11,000 wakiwa wametoweka na idadi ya waliojeruhiwa iliongezeka hadi 171,195.

Tangu Israel ilipoanzisha vita hivyo kwa msaada wa Marekani ya nchi nyingine kadhaa za Magharibi, Wapalestina wapatao 100,000 walilazimika kuondoka Gaza, huku karibu watu milioni mbili wakilazimika kuyahama makazi yao kati ya jumla ya watu milioni mbili na laki mbili waliokuwa wakiishi Gaza kabla ya vita. 

Huko Ukingo wa Magharibi, operesheni za jeshi za Israel na walowezi ziliongezeka na kuua Wapalestina 1,102 na kuwajeruhi wengine 9,034 tangu Oktoba 2023.

Ofisi Kuu ya Takiwmu ya Palestina imesema kuwa kuuliwa shahidi na kujeruhiwa raia wa Palestina kumebadilisha moja kwa moja takwimu za idadi ya watu. Hadi mwishoni mwa mwaka uliomalizika jana wa 2025 idadi ya Wapalestina ilikuwa karibu milioni 5.56, milioni 3.43 walikuwa wakazi wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na milioni 2.13 huko Gaza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *