
Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa mji wa El- Fasher huko Darfur Magharibi nchini Sudan unapitia hali ya kutisha kwa binadamu.
Hali hiyo imebainika baada ya ziara ya kwanza iliyofanywa na Denise Brown, Mratibu Mkazi wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa huko Sudan, huko El Fasher tangu mji huo ulipoangukia mikononi mwa wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) mwezi Oktoba.
Bi Denise Brown amesema kuwa ziara hiyo iliyochukua masaa kadhaa katika mji wa El Fasher imefanyika katika hali ya wasiwasi mkubwa.
Amesema: “Ilikuwa kazi iliyojaa wasiwasi kwa sababau tuliingia katika mazingira tusiyoyajua. Tuliingia katika kile kilichotajwa na Umoja wa Mataifa kuwa eneo lililoshuhudia jinai kubwa”.
Mratibu Mkazi wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa huko Sudan ameongeza kusema, ziara ya mji wa El Fasher imefanyika muda mfupi baada ya kuuawa askari jeshi wa kulinda amani katika eneo jirani la Kadugli.
“Ni idadi ndogo tu ya raia walioonekana wakati wa ziara hiyo, ingawa Umoja wa Mataifa unaamini wengine wengi bado wanashikiliwa au wamejeruhiwa na wanahitaji kuhamishwa haraka kwa ajili ya matibabu”, amesema Denise Brown
Mratibu Mkazi wa Mausala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa huko Sudan amesema vijiji vinavyouzunguka mji El-Fasher vilionekana kutelekezwa kabisa, na kwamba kumeshuhudiwa majengo yaliyoharibiwa au makazi ya muda bila maji safi, vyoo au chakula cha kutosha.