Katika eneo la Garden Park, wilayani Lusaka nchini Zambia, masomo ya lishe bora yanatolewa na wataalamu wa lishe wanaojitolea kwa kushirikiana na wafanyakazi wa Wizara ya Afya ya nchi hiyo.

Mafunzo haya yanalenga kuwawezesha akina mama na walezi kwa kuwapatia ujuzi wa vitendo wanaoweza kuutumia katika maisha ya kila siku. Washiriki hujifunza jinsi ya kuchagua vyakula vyenye lishe vinavyopatikana kwa urahisi katika mazingira wanayoishi, ambavyo si vya gharama kubwa na ambavyo tayari vimezoeleka katika familia zao.

Pia, wanapewa mafunzo ya namna sahihi ya kuandaa vyakula hivyo ili kuhakikisha virutubisho vinaendelea kuwepo hata baada ya kupika.

Mfanyakazi wa kujitolea wa UNICEF nchini Zambia huandaa chakula kwa kutumia jiko linaloweza kubebwa kwa ajili ya programu ya lishe ya watoto.

Mfanyakazi wa UNICEF wa kujitolea anatoa mafunzo kwa kina mama nchini Zambia kwa Ajili ya Programu ya Kulisha Watoto.

Lilian Habeenzu ni Afisa wa Afya na Lishe kutoka Wizara ya Afya ya Zambia, anaeleza ni akina nani wanaolengwa zaidi na mafunzo haya.

“Tunalenga kutoa mafunzo haya kwa akina mama wenye watoto wenye umri wa kuanzia miezi sita hadi miezi 56, lakini tunatoa kipaumbele zaidi kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka miwili ili kukabiliana na tatizo la udumavu.”

Video ya UNICEF Zambia inaonesha afisa lishe wa kiume akielezea kwa kutumia mchoro wa sahani yenye rangi mbalimbali, unaoonesha makundi sita ya vyakula. Anaeleza umuhimu wa kuhakikisha kila mtoto anakula angalau chakula kutoka kila kundi mara kadhaa kwa wiki.

Katika sehemu nyingine ya video, wakina mama wanaonekana wakipata mafunzo ya matumizi ya jiko la kisasa linalotumia nishati kidogo, ni salama na halitoi moshi. Jiko hilo linatumika kuandaa vyakula vyenye virutubisho vya kutosha kwa ajili ya watoto na familia zao.

Mafunzo katika eneo la Garden Park yanahitimishwa kwa washiriki wote kula chakula walichojifunza kukipika, wakionesha furaha na matumaini mapya. Ni mafunzo ambayo si tu yanaboresha lishe, bali yanaweka msingi wa familia zenye afya bora kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *