Arusha. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imetakiwa kuendana na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, kwa kuendelea kutumia na kuboresha mifumo jumuishi ya kikodi hasa ukusanyaji wa kodi za ndani ili kupunguza mianya ya upotevu wa mapato.

Imeelezwa mifumo ya ukusanyaji kodi hasa kodi za ndani itarahisisha ulipaji kodi, kuongeza uwazi, ufanisi na ufuatiliaji wa makusanyo ya Serikali.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Januari 5, 2026 na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar wakati akizungumza katika mkutano wa tathmini ya utendaji kazi wa TRA kwa nusu mwaka wa fedha 2025/2026 ulioanza jijini Arusha leo.

Amesema TRA ina mchango mkubwa ya kujenga nchi na Serikali imeendelea kutekeleza mageuzi mbalimbali ya kiuchumi kwa kuweka sera na mipango mahsusi pamoja na kuboresha mifumo ya ukusanyaji mapato ya Serikali.

Amesema mamlaka hiyo inapaswa kuendelea kutumia mbinu rafiki za kisasa na zenye kuzingatia utu wa mlipakodi katika ukusanyaji wa kodi kwani ukusanyaji wa mapato haupaswi kuwa chanzo cha migogoro bali uwe chachu ya kuongeza uelewa, ushirikiano na uaminifu kati ya TRA na mlipakodi.

“Natoa maelekezo kwa TRA kurahisisha taratibu za kikodi, kupunguza urasimu na gharama zisizo za lazima kwa walipakodi pamoja na kuimarisha majukwaa ya mazungumzo na wadau wa sekta binafsi.

“Katika kuendana na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, naielekeza TRA kuendelwa kutumia na kuboresha mifumo jumuishi ya kikodi itakayopunguza upotevu wa mapato,” amesema.

“Tunasafiri tunafurahia tunayoyaona kwenye mataifa mengine lakini walijitahidi walijitegemea, hawakutegemea sana kwenye mikopo ya nje au kuomba ruzuku. Mjielekeze kuifanya Tanzania kujitegemea kwenye ugharamiaji wa shughuli zake zote na mageuzi makubwa yanayohitajika kimiundombinu katika Taifa letu,” amesema.

Waziri huyo ameagiza wataalamu wa idara ya utafiti washirikiane na wadau na sekta zinazoibukia na kuvutia viwanda ili kuimarisha uchumi zaidi.

Kuhusiana na ongezeko kubwa la makusanyo ya kodi, Waziri huyo amesema tangu mwaka wa fedha 2024/25, TRA ilifanikiwa kukusanya Sh 32.26trilioni ikilinganishwa na Sh 22.2trilioni iliyokusanywa mwaka wa fedha 2021/22 sawa na ongezeko la asilimia 45.

Amesema katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26 (Julai hadi Desemba 2025), TRA ilikusanya Sh18.77 trilioni, sawa na ufanisi wa asilimia 103.7 ya lengo la kukusanya Sh18.10trilioni ufanisi uliochangiwa na makusanyo ya Desemba ambapo TRA imekusanya Sh4.13trilioni.

“Sambamba na hilo, naielekeza TRA kuendelea kupanua wigo wa kodi na kuibua vyanzo vipya vya mapato, hususan katika maeneo ya sekta isiyo rasmi, uchumi wa kidijitali na biashara mtandaoni na huduma mpya na shughuli za kiuchumi zinazokua kwa kasi, hatua hizi zichukuliwe kwa lengo la kuongeza mapato bila kuathiri ukuaji wa uchumi na ustawi wa wafanyabiashara,” amesema.

Awali, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amesema kikao hicho cha tathmini kinawapa fursa ya kuangalia kwa kina maeneo waliyofanya vizuri katika nusu mwaka wa fedha uliopita, kubaini maeneo yanayohitaji kuimarishwa na kujiwekea mikakati ya kuboresha katika kipindi cha fedha kijacho.

Amesema kikao hicho cha siku tano watafanya tathmini na kuweka mikakati kuongeza ufanisi wa mapato,kuboresha huduma na kuimarisha usimamizi wa kodi nchini na kuwa wameendelea kuwa na mshikamano na wadau mbalimbali ikiwemo jumuiya za wafanyabiashara.

Amesema katika kipindi cha Desemba 2025, TRA imeandika rekodi ambayo haijawahi kutokea kwa kukusanya Sh4.1trilioni ambacho kimechangiwa na wananchi wa kawaida, walipakodi wadogo, wakati na wakubwa.

“Katika kipindi cha Desemba tuna vyanzo vinne, walipakodi wakubwa wamechangia kodi ya Sh1.9 trilioni, forodha Sh 1.2 trilioni, wafanyabiashara wadogo na wa kati wakichangia Sh 838bilioni na nyingine ikitoka kwenye kodi ya Muungano,” amesema.

Kamishna huyo amesema wanatarajia kuongeza utoaji huduma,kuboresha mifumo ambapo mwezi huu wanatarajia kuzindua mfumko wa kodi za ndani (IDRAS) ambao utasomana na mifumo mingine ambapo mfumo huo pia utatumia akili mnemba (AI) kama ilivyo baadhi ya mifumo mingine.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Hamisi Livembe, alipongeza TRA kwa kuongeza makusanyo.

“Pamoja na mafanikio mliyopata yanapatikana kwa njia ya maelewano sana tofauti na kipindi cha katikati hapo,tulipitia magumu sana kiasi kwamba ilikuwa ukiona TRA wanapita barabarani unapita chini ya meza, unasema siyo anakuja kwangu?

“Lakini sasa hivi zinakusanywa na kodi zinapatikana kwa njia ya amani sana, katikati hali ilichafuka sana. Kamishna hukuwepo kipindi kile, mahusiano haya yanasaidia kupatikana kwa taarifa mbalimbali,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *