Mwanza.  Shirika la Madini la Taifa (Stamico) limesema upungufu wa upatikanaji wa malighafi ya dhahabu katika Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu Mwanza, unasababisha uzalishaji kuwa chini ya uwezo halisi wa kiwanda hicho.

Hivyo limeiomba Serikali kuingilia kati kwa kuondoa vikwazo vinavyokwamisha upatikanaji wa malighafi hiyo.

Kiwanda hicho kinachomilikiwa na Stamico kwa asilimia 25 na mbia wake kwa asilimia 75, kina uwezo wa kuzalisha kilo 480 za dhahabu kwa siku kwa viwango vya kimataifa.

Hata hivyo, kutokana na uhaba wa malighafi, uzalishaji wake kwa sasa ni kati ya kilo 50 hadi 100 pekee kwa siku.

Katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2025, kiwanda hicho kimenunua dhahabu ghafi kilo 2,995 sawa na tani 2.995 yenye thamani ya dola 305.9 milioni za Marekani.

Ununuzi huo umeiwezesha Serikali kukusanya mrabaha na ushuru wa huduma jumla ya Sh32.4 bilioni.

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatatu Januari 5, 2026 na Katibu wa Stamico, Mudrikat Kiobya, wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji wa kiwanda hicho mbele ya Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk Pius Chaya, aliyefanya ziara katika kiwanda hicho kilichopo eneo la Sabasaba wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Kiobya amesema changamoto ya upungufu wa malighafi inasababishwa na uwepo wa baadhi ya tozo kwa wafanyabiashara wa ndani na nje wanaoingiza madini nchini, ikiwamo ada ya ukaguzi ya asilimia moja, pamoja na kukosekana kwa vituo jumuishi vya utoaji huduma (One Stop Centres) katika mipaka, bandari na viwanja vya ndege.

“Serikali isaidie kuvutia zaidi uingizaji wa madini ya dhahabu nchini kwa kupunguza baadhi ya tozo na kuwezesha uwepo wa vituo jumuishi vya huduma, pamoja na kuvutia uingizaji wa dhahabu ghafi kutoka nje ya nchi,” amesema Kiobya.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dk Pius Chaya (kulia) akimsikiliza mhandisi Noodin Hoja (kushoto) wakati wa ziara yake katika kiwanda cha kusafisha dhahabu Mwanza. Picha na Damian Masyenene

Ameongeza kuwa ni muhimu Serikali kuendelea kuwawezesha wachimbaji na kampuni za madini kuongeza uzalishaji kwa mfumo wa malipo ya awali sambamba na kuhamasisha na kuelimisha wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa kuuza dhahabu zao kwenye kiwanda hicho ili wanufaike na punguzo la mrabaha kutoka asilimia sita hadi nne, pamoja na kufutwa kwa ada ya ukaguzi ya asilimia moja.

Kwa mujibu wa Kiobya, mwaka 2025 kiwanda hicho kimetoa huduma za kusafisha dhahabu jumla ya kilo 7,429 sawa na tani 7.429 kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na wateja wengine, kwa gharama ya Sh2.976 bilioni.

Amesema Stamico na menejimenti ya kiwanda wamejipanga kuendelea kuhamasisha wachimbaji kuuza dhahabu zao katika kiwanda hicho.

Amesema kupitia mpango huo, kiwanda kimechangia kwa kiasi kikubwa kuiwezesha BoT kufikia malengo yake ya kuongeza hifadhi ya dhahabu kwa muda mfupi, hatua itakayoongeza mapato ya kiwanda na mchango wake katika pato la taifa.

“Kiwanda kinaendelea kupokea dhahabu inayonunuliwa na Benki Kuu kutoka kwa wachimbaji na wafanyabiashara, kuifanyia uhakiki wa ubora kabla ya malipo, na kuisafisha kwa ubora wa asilimia 99.999,” amesema Kiobya.

Akizungumzia changamoto hizo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk Pius Chaya amesema Serikali imezipokea na itaendelea kuzifanyia kazi ili kuondoa ukiritimba na usumbufu katika biashara ya dhahabu.

Aidha, ameitaka Stamico kujitangaza zaidi ndani na nje ya nchi ili kuvutia wafanyabiashara wengi wa madini.

Dk Chaya pia ameiagiza Stamico kuharakisha mchakato wa kupata ithibati ya kimataifa, akibainisha kuwa mojawapo ya vigezo ni uwezo wa kiwanda kuzalisha tani 10 za dhahabu kwa mwaka ilhali kwa sasa kinazalisha tani saba pekee.

“Naiagiza Stamico iharakishe upatikanaji wa ithibati ya kimataifa, itangaze kiwanda hiki ndani na nje ya nchi ili kupata malighafi nyingi na iwashirikishe vijana katika uwekezaji wa madini. Lengo la Serikali ni kuvutia wawekezaji na kuifanya Tanzania ionekane kuwa sehemu sahihi na salama ya uwekezaji,” amesema.

Ameongeza kuwa tangu kufanyika kwa marekebisho ya sheria za madini, Stamico imeendelea kufanya vizuri, huku akiipongeza bodi ya wakurugenzi kwa usimamizi wa kiwanda hicho chenye uwekezaji wa Shilingi bilioni 16.5.

“Kuna changamoto tumeziona, lakini tunajivunia biashara kati ya Stamico na BoT ambayo imeongeza mapato ya nchi na kupunguza mlolongo wa watu wanaohusika katika ununuzi wa dhahabu,” amesema.

Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu Mwanza kilifunguliwa rasmi mwaka 2021 na Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni matokeo ya marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017 na kutungwa kwa Sheria namba 5 kuhusu umiliki wa utajiri wa asili na rasilimali za nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *