Kufuatia hatua ya utawala wa Israel ya kulitambua rasmi eneo la Somaliland huko Somalia kama nchi huru, kumetolewa maonyo kuhusu matokeo hatari ya kisiasa na kiusalama ya kitendo hicho.

Hatua ya Israel ya kutambuwa rasmi eneo la Somaliland kama nchi huru imekabiliwa na upinzani mkali katika ngazi za kikanda na kimataifa kuhusu matokeo hatari ya kisiasa na kiusalama ya kitendo hiki. Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud ameonya kwamba: Israel inataka kuwahamisha kwa mabavu Wapalestina na kuwapeleka Somalia na inakusudia kudhibiti njia za kimkakati za majini. Kujikurubisha Israel kwa Somaliland hakufanyiki kwa malengo ya amani. Sheikh Mahmoud anafafanua kwa kusema: “Israel imekuwepo Somaliland kwa muda sasa, na kutambua rasmi nchi huru ya Somaliland ni jitihada za kuanzisha uhusiano rasmi uliokuwepo kwa siri.” Rais wa Somalia ameendelea kusema: “Somaliland imekubali kuwawepokea Wapalestina wanaofukuzwa na Israel katika nchi yao, kujenga kambi ya utawala huo, na kujiunga na Makubaliano ya Abraham.”

Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini imetoa taarifa ikieleza wasiwasi wake kuhusiana na hatua hiyo ya utawala wa Kizayuni wa Israel ikisisitiza kwamba, kutambua rasmi Somaliland kama nchi huru kunakiuka mamlaka ya kitaifa na umoja wa ardhi ya Somalia na kuonya kwamba uamuzi huo wa utawala wa Israel ni “tishio la moja kwa moja” kwa amani katika Pembe ya Afrika. Taarifa hiyo imesema: “Kitendo cha Israel kinaunga mkono hatua za kujitenga na kinatia nguvu harakati za kuteteresha amani na utulivu.” Afrika Kusini imesema kwamba inaunga mkono kanuni ya Umoja wa Afrika ya kuheshimiwa mipaka iliyoanzishwa wakati wa uhuru ili kuzuia migogoro, na imetoa wito kwa jami ya kimataifa “kupinga uingiliaji kati wa Tel Aviv katika masuala ya ndani ya Somalia na kuunga mkono Somalia moja na yenye utulivu.”

Inaonekana kwamba kitendo cha Israel cha kutambulia rasmi eneo la Somaliland kama nchi huru kinaweza kuwa na athari mbaya za kisiasa na kiusalama katika Pembe ya Afrika na hata maeneo ya mbali zaidi. Uamuzi huu sio tu kwamba unatishia mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi ya Somalia, lakini pia utafungua njia ya kuongezeka mivutano ya kikanda na harakati za makundi yenye misimamo mikali.

Israel ndio utawala wa kwanza kabisa kutambua rasmi eneo la Somaliland lililotangaza kujitenga na Somalia kama nchi huru. Somaliland ilijitangazia uhuru mwaka 1991 baada ya kuanguka serikali kuu ya Somalia na imekuwa ikiendeshwa kama taifa kwa miongo mitatu iliyopita. Hata hivyo, hadi sasa jamii ya kimataifa imekataa kuitambua rasmi kutokana na kanuni ya kulindwa mipaka ya zama za kikoloni, na wasiwasi kuhusu uwezekano wa hatua kama hiyo kuhamasisha harakati zingine za kujitenga. Uamuzi wa Israel umevunja mwafaka huo na kuibua mgogoro mpya wa kidiplomasia katika Pembe ya Afrika.

Kwa mtazamo wa kisiasa, hatua hii inayumbisha moja kwa moja mamlaka ya kujitawala ya Somalia na inaweza kudhoofisha serikali kuu huko Mogadishu. Serikali ya Somalia imeutaja uamuzi huo kuwa ni “shambulio la wazi dhidi ya umoja wa kitaifa” na kinyume cha sheria. Nchi nyingi duniani pia, zimetangaza upinzani wao mkubwa dhidi ya hatua hiyo ya Israel.

Kwa mtazamo wa kiusalama, uwepo wa utawala wa Kizayuni wa Israel huko Somaliland utasababisha ukosefu wa amani na ongezeko kubwa la mivutano katika Pembe ya Afrika na Bahari Nyekundu. Katika suala hili, harakati ya Ansarullah ya Yemen imetangaza kwamba itautambua uwepo wowote wa Israel huko Somaliland kama shabaha halali ya kijeshi. Vitisho hivi vinaweza kusababisha makabiliano ya kijeshi na ukosefu wa usalama katika eneo hilo. Zaidi ya hayo, Somaliland haina udhibiti kamili wa maeneo yake yote inayodai kuwa ni malki yake na inakabiliwa na upinzani na uasi wa ndani katika sehemu kama vile majimbo ya Sool na Sanaag. Kuingia Israel katika mazingira kama haya kunaweza kuzidisha machafuko na kufungua njia ya migogoro mipana ya ndani.

Katika upande mwingine, nafasi ya jiografia ya kisiasa ya Somaliland karibu na lango bahari la Bab el-Mandeb na Bahari Nyekundu ina muhimu sana. Eneo hili ni mojawapo ya njia muhimu zaidi za meli duniani, na uwepo wowote wa kijeshi wa Israel katiika eneo hilo unaweza kuzidisha ushindani wa kijeopolitiki. Nchi za kanda hiyo zina wasiwasi kwamba hatua hiyo ya Israel itapelekea kuanzishwa vituo vya kijeshi vya utawala huo kwenye pwani ya Somaliland, na kutishia usalama wa baharini.

Kwa ujumla, inapaswa kusemwa kwamba, hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel kutambua rasmi Somaliland kama nchi huru imeibua mgogoro mpya wa kidiplomasia barani Afrika, na kuzidisha hatari kubwa za kiusalama kwa Somaliland, Somalia na eneo lote la Pembe ya Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *