Dar es Salaam. Haya majina na warembo ni kama pipi na watoto ama kitunguu na nyanya. Vinywa vyao viliumbwa kwa kazi ya kuzimua masikio ya wanawake. Wanaimba tena sana na wanapendwa tena sana. 

Kila mmoja kwa wakati wake. Vipi unamkumbuka Aslay aliyeachia mashabiki waimbe wenyewe zile ngoma kila alipoenda? Ni wazi muziki ni kama una mashetani na mapepo ndani yake.

Unamkumbuka Jay Melody hapo katikati? Kila pisi alitamani kuwa pisi ya Jay Melody. Lakini hii leo Jay Melody ni kama wa kumsaka kwa tochi kama siyo kurunzi. Huu muziki una giza sana.

Kandokando ya Aslay kasimama Mbosso. Katikati ya Jay Melody kuna Marioo kutoka ‘Alooo’. Hao ni kama wamepokezana namna flan kuwatumikia mashabiki wao. Fuatilia kwa umakini.

Si kwamba Aslay na Jay Melody sasa wanaishi kwa kazi mpya. Hapana wanaendelea kutegemea muziki huo huo. Tofauti yao hapo ni kubwa sana mpka uzame ‘dipu’ kufukunyua. 

Ni kwamba muziki unamtegemea Marioo. Wakati Jay Melody sasa anautegemea muziki. Ndo Aslay, leo anategemea muziki na wakati muziki ukimtegemea Mbosso. Hii iko wazi.

Marioo kama ilivyo kwa Mbosso, wanaweza kuishi vizuri bila hata kutegemea ‘hits song’. Na maisha haya pia waliyaishi Jay Melody na Aslay. Yaani unakuwa juu mpaka muziki ubakuheshimu.

Haya maisha aliyaishi Inspekta Harun ‘Babu’. Miaka ya 2001 na mpaka 2005. Juma Nature na wengineo. Lakini leo hii muziki hauwategemei wao, bali wao ndo wanategemea muziki.

Diamond kitambo sana aliachana na pigo za kutegemea muziki. Ila muziki unamtegemea yeye kwa muda mrefu. Ni kwamba ngoma za Mondi zinaupaisha muziki wa Bongo zaidi. 

Wakati hapo nyuma muziki ndiyo uliompaisha Mondi. Ni kama vile Aslay, kila ilichogusa kilieguka almasi. Kwa sasa anautegemea muziki kuliko muziki kumtegemea yeye.

Kwa sasa vijana wawili Marioo na Mbosso wameuteka muziki huu. Wao ndo wanatoa maelekezo ya wapi muziki uende. Nieleweke kwamba naongelea wasanii wa daraja lao.

Wakati Aslay anatamba, alikuwa na daraja lake. Tofauti na Mondi, Kiba, Darassa na wengine. Hata leo kina Mbosso na Marioo, ni daraja la nyuma ya Konde, Kiba, Mondi au Van Boy. 

Hata nyakati zile muziki ulikuwa na madaraja. Alipo Profesa Jay usingewakuta wasanii kama Pig Black na D Knob. Alipo Jide katu asingekuwepo Sister P na Zay B.

Ndivyo ilivyo kwa Nature na Q Jay na wenzake. Kwa sasa lipo daraja la Marioo na Mbosso, na daraja la Diamon na Konde na wengineo. Ila kwa daraja lao hao ndio alama sahihi. 

Utaajiuliza kwanini Jay Melody hivi sasa hatajwi kama Marioo? Au Aslay kwanini hatoi ngoma mara kwa mara kama Mbosso? Muziki una mapepo flan ambayo ili uyaelewe lazima uwe pepo na wewe.

Aslay ana sauti ileile na uwezo wa kuimba uleule. Lakini hayupo kwenye ‘paipu laini’ kwa sababu zisizo na sababu. Hata yeye pia wakati yupo juu, Q Chief hakuwa juu kwa sababu bila sababu.

Jay Melody unadhani kabadilika kwa sauti na sura? Hapana hata kwa kuandika na kuimba ni yule yule. Lakini sababu ya kukosa kukaa kwenye ‘meini striimu’ haina sababu. 

Leo Marioo hata akiumwa ‘fluu’ ni stori kubwa. Kwa sababu huu ni wakati wake sahihi na anafanya mambo makubwa. Ndivyo ilivyo kwa Mbosso mbele ya Aslay na wengineo. 

Ndo maana kuna wakati watu wanapaswa ‘kushoo rispekti’ kwa mtu kama Mondi. Kwa sababu ni miongoni mwa wanamuziki wa kizazi kipya waliodumu muda mrefu.

Kuna kudumu muda mrefu kwa uhai wa maisha. Kuna kudumu muda mrefu kwa ubora wa kazi zako na kuna kudumu sana kwa kuwepo kwenye ‘mainstream’ muda mrefu.

Mondi kwenye hili kajimilikisha utawala wa kidikteta. Anafanya anavyotaka na watu wanafuata. Kuna kipaji na karama, Mondi anavyo vyote kipaji na karama. Na hii siyo kwa kila mtu. 

Jay Melody, Marioo, Aslay na Mbosso wana utawala wao hao. Wamejimegea kipande chao cha kutafuna nchi. Jay Melody wa sasa siyo wa kushinda studio kama anasubiri umeme wa luku.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *