Mara. Serikali mkoani Mara imetoa siku 21 kwa wakuu wa wilaya za mkoa huo kuhakikisha watendaji wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) wanapata ofisi za uhakika na za kudumu hasa katika majengo ya Serikali.
Akitoa maagizo hayo leo Jumanne Januari 6,2026 mjini Musoma, Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi amesema kuwa ofisi nyingi za Tarura mkoani humo kwa ngazi za wilaya zipo katika majengo ya watu binafsi jambo ambalo kwa namna moja ama nyingine linakuwa kikwazo kwa utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo ya Serikali.
Kabla ya kutoa agizo hilo, Meneja wa Tarura Mkoa wa Mara, William Gyunah amesema miongoni mwa changamoto wanazokutana nazo katika kutekeleza majukumu yao ni pamoja na kutokuwa na ofisi katika baadhi ya wilaya.
Gyunah ametaja wilaya ambazo hazina ofisi na kulazimika kupanga kwenye nyumba za watu binafsi kuwa ni pamoja na Serengeti, Rorya na Tarime.
“Maeneo mengi tumepanga kwenye majengo ya watu binafsi hivyo tunashindwa kufunga mifumo au mitambo ya serikali kule hali hii kwa namna moja ama nyingine inakuwa ni kikwazo kwetu katika kutekeleza majukumu yetu,” amesema
Baadhi ya wajumbe wa kikao cha bodi ya barabara mkoani Mara wakiwa kwenye kikao mjini Musoma. Picha na Beldina Nyakeke
Kutokana na maelezo hayo,Kanali Mtambi amesema miundombinu hasa barabara ni jambo muhimu katika kuchochea maendeleo hivyo hakuna sababu ya kuwepo kwa vikwazo katika kuifanya miundombinu hiyo kuwa bora na inayopitika muda wote.
“Hili la ofisi lipo chini ya uwezo wenu wakuu wa wilaya, natoa siku 21 kila wilaya kuwe na ofisi ya Tarura kwenye majengo ya Serikali ili waweze kufunga mifumo yao kwaajili ya kutekeleza majukumu yao kwani haiwezekani kufunga mifumo hiyo kwenye maeneo yasiyo rasmi,” amesema
Katika kikao hicho, wajumbe pia wameitaka Serikali kuu kutoa fedha za kutosha kwaajili ya utekelezaji wa miradi ya barabara tofauti na ilivyosasa ambapo wamedai fedha inayotolewa haifiki nusu ya bajeti inayotengwa ingawa hawakutoa takwimu halisi.
Mbunge wa Bunda Mjini Ester Bulaya amesema kutokukamilika kwa miradi mikubwa ikiwepo miradi ya kimkakati ni ishara ya Serikali kutokutoa fedha ya bajeti kwa asilimia 100.
Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa uwanja wa ndege Musoma ulioanza mwaka 2021 na ulitarajiwa kukamilika Desemba 2022 kwa gharama ya Sh35 bilioni lakini hadi sasa mradi huo bado haujakamilika na upo asilimia 58 za utekelezaji wake.
Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara amesema miradi mingine iliyoshindwa kukamilika kwa wakati ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Tarime- Mugumu yenye urefu wa kilomita 87.14
Mbunge wa Viti Maalum, Ghati Chomete amesema ipo miradi ambayo imeshindwa kuanza licha ya Serikali kuahidi kuifanyia kazi ikiwepo barabara ya Musoma- Busekekela na Mika – Kirongwe wilayani Rorya.
Akizungumzia suala hilo,Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi amesema maombi hayo yatafikishwa Serikali kuu ili fedha zitolewe kwaajili ya utekelezaji wa miradi ya barabara kwa maelezo kuwa hali ya barabara mkoani humo bado siyo ya kuridhisha.
“Sera inasema makao makuu ya Mkoa lazima yaunganishwe na makao makuu ya wilaya kwa lami vile vile makao makuu ya wilaya moja lazima yaunganishwe na makao makuu ya wilaya jirani lakini hali ni tofauti mfano kwa wilaya za Rorya na Serengeti zeneywe hazijaunganishwa na shemuenyoyoye yaani mkoani wala wilaya jirani,” amesema Kanali Mtambi. Andika vichwa vya habari