MJANE wa Baba wa Taifa, Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere ametoa wito kwa Watanzania kudumisha mshikamano na kutumia mazungumzo kama njia pekee ya kuvuka changamoto zinazolikabili taifa kwa sasa.
Akizungumza nyumbani kwake Msasani, Dar es Salaam, Mama Maria amewataka Watanzania kutokata tamaa, bali kutambua hatua ambazo nchi imepitia tangu enzi za Nyerere.
Mama Maria alisema nchi imepitia katika makundi matatu, akisisitiza kila kizazi kina deni kwa taifa lake.
“Kundi la Kwanza lilipigania na kuleta Uhuru wa bendera, likiongozwa na waasisi wa taifa hili. Kundi la pili lilijenga misingi ya nchi, kuweka mifumo ya utawala na huduma za kijamii na kundi la tatu ni kizazi cha sasa, ambacho kina jukumu la kuendeleza na kuona mwanga mkubwa zaidi wa maendeleo.” alisema.
Aliongeza: “Msikate tamaa. Tunachohitaji ni kukubaliana wote, tukae chini na kuzungumza ili kuelewana namna ya kuifikisha nchi mbele.”
Kauli ya Mama Maria imekuja wakati ambapo taifa limekuwa likishuhudia vuta nikuvute katika nyanja za kijamii na kiroho lakini akasisitiza kuwa ujenzi wa taifa si kazi ya mtu mmoja au kiongozi pekee, bali ni matokeo ya maelewano ya pamoja.
Amewasihi vijana kutokata tamaa kutokana na changamoto za sasa, bali watumie mawazo yao kuleta mabadiliko chanya bila kusubiri kulaumu wengine.
Kauli hiyo ameitoa wakati akipokea nishani ya heshima iliyotolewa na serikali ya Angola kwa Nyerere, kama ishara ya kuthamini mchango wake katika ukombozi.
Nishani hiyo ilikabidhiwa kwake na Balozi wa Angola nchini, Domingos Da Silva na kushuhudiwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
