
Josep Borrell, mwanadiplomasia mkuu wa zamani wa Umoja wa Ulaya (EU) amesema, kambi hiyo inapaswa iache kuichukulia Marekani kama mshirika wake mkuu, huku Washington na Brussels zikiwa zinazozana hivi sasa kuhusu sera za kidijitali na udhibiti wa eneo la Greenland.
Borrell ameeleza hayo katika mahojiano na mtangazaji wa chaneli ya Antena 3 ya Uhispania na akafafanua kwa kusema: “sijui ni kipi zaidi [Rais wa Marekani Donald] Trump anahitaji kufanya ili sisi tuelewe kwamba Marekani na Ulaya si washirika kama walivyokuwa hapo kabla”.
Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, mkuu wa zamani wa sera za nje wa EU amezungumzia wasiwasi ulioonyeshwa na Trump kwamba mataifa yenye nguvu za nyuklia barani Ulaya – Ufaransa na Uingereza – siku moja yanaweza kuwa na serikali ambazo si rafiki kwa Washington; na akasema: “kuna watu wengi ambao hawataki kukubali ukweli huu kwa sababu ingali inadhaniwa kwamba Marekani ndiyo mshirika mkuu wa EU, lakini si hivyo tena”.
Akigusia shambulio la kijeshi la Marekani dhidi ya Venezuela, Borrell amesema, uingiliaji huo wa kijeshi uliofanywa na Marekani inapasa uwe ni “somo kwa watu wa Ulaya”; na akaongezea kwa kusema: “kwa sababu ikiwa tunataka tuwepo duniani, [sisi] tunapaswa pia kuwa na uwezo wa kiwango fulani wa kujilinda, na si kutegemea atulinde rafiki Marekani”.
Borrell ametoa maoni hayo wakati Trump anatilia mkazo madai yake kwamba, Marekani inapasa “bila shaka yoyote” iidhibiti Greenland kwa sababu za usalama wake wa taifa, huku Ikulu ya White House ikibainisha kwamba kulitumia jeshi la Marekani “daima linabaki kuwa chaguo” la kufanikishia lengo hilo…/