Marekani imeongeza vitisho vya kutaka kuichukua Greenland kisiwa cha kimkakati kilichopo kwenye eneo la Bahari ya Arctic kinachomilikiwa na Denmark. Kutokana na msimamo mkali wa utawala wa Rais Donald Trump, Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, amesema hatua kama hiyo itaashiria mwisho wa muungano wa kijeshi wa NATO.
Mara baada ya Trump kutumia nguvu za kijeshi nchini Venezuela, alianza kugonga kengele ya tahadhari barani Ulaya kwa kurudia msisitizo wake kwamba anataka kuchukua udhibiti wa Greenland.
Eneo hilo lenye utajiri wa madini lenye mamlaka ya kujitawala kwa kiasi ni sehemu ya Denmark ambayo ni mshirika wa jumuiya ya kijeshi ya NATO na mshirika wa muda mrefu wa Marekani, iliyo na kambi ya kijeshi nchini humo, limekuwa linamdondosha mate Trump tangu muhula wake wa kwanza madarakani.
Tangu kurejea madarakani mwezi Januari mwaka uliopita, Trump alilifufua wazo lake juu ya kukidhibiti kisiwa hicho, akitaja umuhimu wake wa kimkakati kwa ulinzi na pia kwa utajiri wake wa madini. Na sasa utawala wa Trump umeongeza kusisitiza kwamba “kuinunua Greenland ni kipaumbele cha usalama wa taifala Marekani”.
Trump anajadili njia tofauti za kutimiza lengo lake Greenland
Rais Trump na maafisa wake wanajadili njia mbalimbali za kulifikia lengo hili muhimu la sera za kigeni za Marekani, na wamesema bila shaka, kutumia nguvu za kijeshi kwa Marekani daima jambo hilo lililopo mezani.
Ingawa Trump alikuwa alitumia nguvu za jeshi la Marekani dhidi ya adui yake wa muda mrefu Venezuela, lakini kutumia nguvu dhidi ya mshirika wake wa karibu kama Denmark itakuwa ni hatua tofauti.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema hataki hata “kufikiria hali hiyo” ambayo Marekani itakiuka uhuru wa Denmark. Amesema kitendo chochote cha kijeshi cha Marekani dhidi ya Greenland kitauvunja muungano wa kijeshi wa NATO.
Kifungu cha Tano cha sheria za NATO ni kwamba wanachama watalindana iwapo mmoja wao atashambuliwa, kifungu hicho kinalenga kuzuia vitisho kutoka nje na hivyo wazo la mshirika mkuu Marekani kutumia nguvu yake kumgemgeukia mshirika mwenzake linaonekana kuwa lisiloweza kufikirika.
Chini ya makubaliano yaliyopo na Denmark, Marekani inaweza kuwaweka wanajeshi wake zaidi katika kisiwa cha Greenland ikiwa inataka.
Rubio: Trump anataka kuinunua Greenland badala ya kuishambulia
Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amewaambia wabunge kuwa Trump anataka kuinunua Greenland badala ya kuishambulia na kwamba matumaini ya jumuiya ya NATO ni kwamba diplomasia itasimama.
Spika wa Bunge: Mike Johnson, amesema hadhani kama kuna yeyote anayezungumzia kuhusu hatua za kijeshi huko Greenland,ila zinanaangaliwa njia za kidiplomasia.”
“Marekani wakati wote huwa na uwezekano wa kuchagua kutumia njia ya kijeshi kwa kila kitu. Nadhani hii ni kauli ya jumla. Lakini kuhusu Greenland, ni wazi kabisa tunaegemea zaidi njia za kidiplomasia.”
Kuna hofu kwamba kwa Marekani kuongeza uwezekano wa kumshambulia mshirika au kuishinikiza nchi mwanachama wa NATO kuiachia eneo lake Marekani inaweza kuwa tayari imeivuruga NATO.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot amesema nchi yake inazungumza na Ujerumani na Poland ili kuja na mpango wa kukabiliana na uwezekano huo.