Alhamisi ya wiki hii raia wa Uganda, watapiga kura kuchagua rais, wabunge na wawakilishi wengine, katika uchaguzi ambao karibu robo tatu ya raia wa nchi hiyo wenye umri wa miaka 40, wamekua wakimjua rais mmoja tu katika maisha yao.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Kwa raia waliozaliwa miaka 40 iliyopita, kwao rais ni mmoja tu waliyemshuhudia, si mwingine bali ni Yoweri Kaguta Museveni, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 81 na baada ya kuwa madarakani kwa karibu miongo minne, anataka kuchaguliwa kwa muhula wa 7.

Wafuasi wake wanamsifu kwa kile wanasema ameleta utulivu, ukuaji wa uchumi na amani baada ya miaka kadhaa ya utawala wa  Iddi Amini na Milton Obote, hata hivyo wakosoaji wanasema tangu yuko madarakani amedhoofisha pakubwa taasisi za serikali, kunyamazisha wapinzani wake na kubadili sheria mara kwa mara kumpendelea.

Wafuasi wa chama tawala nchini Uganda- NRM wakati wa kampeni.
Wafuasi wa chama tawala nchini Uganda- NRM wakati wa kampeni. REUTERS – Abubaker Lubowa

Rais Museveni ambaye wakati mmoja alikuwa mkosoaji mkubwa wa viongozi wenzake waliokaa madarakani kwa muda mrefu, sasa anakuwa miongoni mwao baada ya kufanya marekebisho ya sheria mwaka 2005 kuondoa ukomo wa rais kukaa madarakani na baadae mwaka 2017 kuondoa kipengele cha makataa ya umri wa rais.

Viongozi wa upinzani kama Kizza Besigye na muimbaji aliyegeukia siasa Robery Kyagulani, wamekamatwa mara kadhaa, kupigwa na hata kufunguliwa kesi kubwa kama inayomkabili hivi sasa Kizza Besigye anayeshtakiwa kwa uhaini.

Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu wa urais wa mwezi huu.
Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu wa urais wa mwezi huu. REUTERS – Abubaker Lubowa

Kuelekea uchaguzi huu tayari mashirika ya kutetea haki za binadamu na umoja wa Mataifa, yameeleza kuguswa na ukiukwaji wa haki za binadamu kunakofanywa na vikosi vya usalama dhidi ya wafuasi na wagombea wa upinzani, taasisi hizo zikionya kuwa uchaguzi wa Januari 15 hautakuwa huru, haki na kuaminika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *