Nchini Uganda, Idara ya usalama imesema imejiandaa vilivyo kukabiliana na vitisho vyote vya usalama kuelekea uchaguzi mkuu wa siku ya Alhamisi, huku Tume ya Uchaguzi ikisema iko tayari kwa zoezi hili.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Katika hatua nyingine, mgombea mkuu wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, anayepambana na kiongozi wa muda mrefu Yoweri Museveni, amealiambia Shirika la Habari la AFP kuwa, ataitisha maandamano iwapo kutakuwa na wizi wa kura.
Katika kikao cha pamoja kati ya tume ya uchaguzi ,waangalizi wa kimataifa na idara ya usalama, Inspekta Jenerali wa Polisi Abbas Byakagaba ametumia fursa hiyo kutangaza maandalizi ya usalama ikiwemo kushirikisha vikosi maalum na vikosi vyote vya usalama.
“Tumezingatia pia wakati huu vitisho vingine vya usalama vikiwemo ugaidi, machafuko wakati mikutano ya kisiasa,uchochezi ,fujo kwenye vituo vya kura,na hata propoganda za vyombo vya habari.Tuna mkakati wa kuwatuma vikosi vyetu na nisisitize polisi wataongoza na kusaidiwa na vikosi vingine.” alisema Inspekta Jenerali wa Polisi Abbas Byakagaba.
Kwa upande wake mwenyekiti wa tume ya uchaguzi alielezea kuwa tume hiyo itafanya juu chini kuzingatia sheria za uchaguzi na uchaguzi wa amani.
Timothy Chemonges mchambuzi wa masuala ya kisiasa anazungumzia uchaguzi huo wa Uganda.
“Kwa ujumla kampeni zimeendelea vizuri bila vurugu nyingi kama uchaguzi uliopita,naamini kwa ujumla kutakuwa na amani,hata hivyo kuna uwezekano wa kuzimwa mtandao na baadhi ya wanasiasa wa upinzani kuweka kwenye aina fulani ya udhibiti au ufuatiliaji wa karibu nyumbani.” amesema Timothy Chemonges mchambuzi wa masuala ya kisiasa.
Japo raia wanasema kuna usalama ,kuna baadhi ambao wamekwepa mijini wakihofia usalama wao.