Alhamisi hii rais wa Uganda Yoweri Museveni atakuwa katika jaribio jingine la kutaka raia wa nchi hiyo wamuongezee muda zaidi wa utawala wake uliodumu kwa karibu miongo minne, uchaguzi ambao uimeibua tena maswali kuhusu urithi wa uongozi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Museveni ambaye aliingia madarakani mwaka 1986 baada ya kuongoza mapinduzi, anagombea kwa muhula wa 7, huku mpinzani wake mkuu mwenye umri wa miaka 43 Bob Wine, ambaye alimaliza wapili katika uchaguzi wa mwaka 2021 kwa kupata asilimia 35, anafurahia uungwaji mkono mkubwa wa vijana.
Katika uchaguzi huu kuna wagombea wengine 8 wanaotaka raia wa Uganda wawachague akiwemo afisa wa zamani kwenye jeshi la Uganda, Mugisha Muntu na mbunge Nandala Mafabi aliyekuwa kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni.
Katika kampeni za mwaka huu ajenda kuu ya rais Museveni imekuwa kulinda amani na mafanikio ambayo nchik imepata chini ya utawala wake, akisisitiza kuifanya nchi hiyo kuwa ya kipato cha kati, huku mpinzani wake Bob Wine ajenda yake kubwa imekuwa kurejesha uhuru wa kisiasa na kutengeneza ajira kwa vijana, akimshutumu Museveni kuongoza nchi hiyo kwa mkono wa chuma kwa miaka 40.
Aidha suala la usalama limesalia kuwa kipaumbele kuelekea uchaguzi wa Alhamisi, ambapo katika chaguzi zilizopita kulishuhudiwa vurugu za hapa na pale, ikiwemo kuuawa kwa watu karibu 50 katika uchaguzi wa mwaka 2021 baada ya Bob Wine kukamatwa.
Kuelekea uchaguzi huu mamia ya wafuasi wa upinzani wamekamatwa na vyombo vya usalama, huku jeshi kuhusishwa kwa kiasi kikubwa kwenye siasa za mwaka huu, kukiibua maswali kuhusu uhuru wa uchaguzi wenyewe.
Uchaguzi huu pia unafuatiliwa kwa karibu na waangalizi wa ndani pamoja na washirika wa kigeni, hasa ukizingatia kuwa katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2021, Marekani na waangalizi wa umoja wa Ulaya walisema haukuwa, wa huru, haki wala wa kuaminika.
Licha ya kuwa ushindi wa rais Museveni kwenye uchaguzi huu ni hakika, wachambuzi wa mambo wanasema tofauti ya kura baina ya wagombea wawili wakuu, itaamua mustakabali wa baadae wa kisiasa wa taifa hilo.