Wananchi Mirerani wakosa maji siku saba, bei yapaaWananchi Mirerani wakosa maji siku saba, bei yapaa

WAKAZI wa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wako katika hali mbaya kwa zaidi ya siku saba baada ya huduma ya maji safi na salama ya kunywa kukosekana kwa muda huo.

Hiyo ni baada ya malori yanayouza maji hayo kutoka Mji mdogo wa Bomang’ombe wilayani Hai mkoani Kilimanjaro kudaiwa kuzuiwa.

Kwa zaidi ya miaka 20 wakazi wa Mirerani, wanatumia maji ya kunywa yanayouzwa na malori kutoka mji mdogo wa Bomang’ombe wilayani humo.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wakazi wa Mirerani wanatumia maji ya visima vifupi na virefu kwa kunywa na huduma nyingine huku wakiendelea kulalamika kukosa maji ya kunywa kutoka Bomang’ombe.

Akizungumzia hali hiyo katika Mji wa Mirerani, mwananchi Andrew John amesema kwa zaidi ya miaka 20 walikuwa wanatumia maji ya kunywa yanayotoka Bomang’ombe, Hai ila wanasikitishwa hivi sasa kupata zuio hilo wakati wote ni Watanzania.

“Hivi sasa kuna baadhi ya malori machache yamefanikiwa kuleta maji Mirerani ila ndoo moja ya lita 20 ya maji ya kunywa tunauziwa Shilingi 2,000 badala ya Shilingi 1,000 kama awali,” alisema. Mmoja wa wauza maji wa eneo hilo, Abdi Soka alisema watu wengi wameathirika kwa ukosefu wa maji kutokana na zuio la baadhi ya viongozi wa serikali wilayani Hai.“Wanaoleta maji na kutuuzia kupitia malori kutoka Bomang’ombe wamedai viongozi wa serikali wamezuia malori hayo yasilete maji Mirerani,” alisema Soka.

Meneja wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA) Mirerani, Fidelis Shayo ameeleza kwamba hata yeye amesikia changamoto ya maji hayo kukosekana katika mji huo wenye sifa ya kuchimba madini ya Tanzanite duniani.

Shayo alisema AUWSA haihusiki kuzuia huduma ya maji kutoka maeneo mengine japokuwa mradi wao wa maji wa Mirerani unaendelea kutoa huduma kwa uhakika maeneo hayo maji safi na salama.

“Maji ya AUWSA Mirerani ni safi na salama kwani yametibiwa kwa dawa, tunaendelea kuwasihi watu wa eneo hilo waendelee kutumia hata kwa kunywa ndiyo sababu serikali imetenga Shilingi bilioni 4.3 kwa ajili ya mradi wa maji Mirerani,” alisema Shayo.

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Hassan Bomboko alipoulizwa kwa njia ya simu juu ya suala hilo alisema wenye mamlaka ya kulizungumzia suala hilo ni viongozi wa serikali Mirerani na si yeye.

“Kama upo huko Mirerani waulize viongozi wa huko juu ya suala hilo na wanaweza kukupa taarifa nzuri lakini mimi siwezi kulizungumzia kwa sasa,” alisema Bomboko.

Naye Ofisa Mtendaji wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani (TEO), Isack Mgaya alisema kwa sababu suala hilo lipo nje ya Wilaya ya Simanjiro wameshindwa kuingilia kati.

“Tulipata taarifa kuwa uongozi wa Hai umezuia maji hayo kwa madai kuwa ni machache kwao ila tumefikisha suala hilo kwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Lulandala ili azungumze na uongozi wa Hai,” alisema Mgaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *