Rais Samia ametoa kauli hiyo hii Jumanne jijini Dodoma wakati akihutubia katika mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Mahakimu na Majaji, TMJA, akisema kuwa uwepo wa mahakama huru yenye uwezo na uadilifu ni nguzo muhimu na ni msingi wa upatikanaji wa haki na kwamba serikali itaendelea kuulinda licha ya baadhi ya watu kufungwa kwa kesi ya kubambikiwa:
“Watanzania wana matumaini makubwa sana na nyinyi na wangependa kuona mahakama inasimamia haki kwa uwazi na kwa kuzingatia misingi ya kikatiba, kisheria lakini vilevile utu. Huku mahabusu kuna mtu anafungwa kwa kesi ya kubambikiwa tu.,” alisema Rais Samia.
Awali akizungumza katika mkutano huo Jaji Mkuu George Mcheche Masaju amesema kuwa mahakama haiwezi kuwa huru endapo watendaji wake hawana uhakika wa mishahara, posho, pensheni pamoja na usalama wao. Amesema “Mheshimiwa rais mahakama haiwezi kuwa huru endapo watendaji wake hawana uhakika wa mishahara yao, posho, pensheni, usalama…”
Akaongeza “Mambo mengine mheshimiwa rais yanasikitisha lakini majaji waliostaafu.. kwanza tu wanaostaafu wanachelewa baada ya kuhamishwa kutoka kwenye mfuko mkuu wa hazina kama katiba inavyoelekeza..” alisema Jaji Masaju.
Kauli ya Samia yapokelewa kwa mitizamo tofauti
Hata hivyo, kauli hii ya Rais Samia imepokelewa kwa utata mkubwa. Lawama za watu kubambikiwa kesi si mpya sio tu kutoka kwa jamii, bali hata mwenyewe Rais Samia si mara ya kwanza kuzitaja. Kuna wakati alifika hata kuunda tume ya haki jinai iliyoongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu Othman Chande kuchunguza madai hayo.
Lakini kwa wengi, kuendelea kuwapo kwa ukandamizaji huu ni kutokana na sababu za kisiasa kuingizwa kwenye utendaji wa vyombo vya dola, hasa jeshi la polisi. Rais wa Chama cha Mawakili, TLS, Wakili Msomi Boniphace Mwambukusi amesema kauli kama hizi kwa sasa zimepitwa na wakati na kinachotakiwa sasa ni vitendo, akigusia pia suala la Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, aliyeko mahabusu kwa kesi ya uhaini.
Alisema “Tumezungumza sana, tumeahidi sana, lakini hizi hotuba… kwa sasa watu wanataka kuona kwa vitendo. Na kuna mambo ya kuonyesha haki kwa sababu moja ya mtu ambaye yuko ndani kinyume cha sheria ni Tundu Antipas Lissu..”
Sekta ya haki nchini Tanzania kwa muda mrefu imekuwa ikitupiwa lawama kwa kushindwa kutekeleza kikamilifu masuala ya utoaji haki.
