RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi aliowateua hivi karibuni wakiwemo mawaziri na naibu mawaziri wakatekeleze kwa wakati ahadi zilizotolewa kwa wananchi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.
Alitoa maelekezo hayo wakati akiwaapisha viongozi hao aliowateua hivi karibuni wakiwemo mawazi, naibu mawaziri, katibu mkuu na mabalozi katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Dodoma.
“Nawapongeza kwa uteuzi na mkatimize majukumu yenu kwa kuzingatia viapo vyenu, na mkatekeleze kwa wakati ahadi zilizotolewa kwa wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu,” alisema.
Rais Samia amesema mabadiliko ya uongozi ni sehemu ya utaratibu wa kawaida wa kuboresha utendaji wa serikali na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi, na kwamba uteuzi wa viongozi hao umezingatia uwezo, uzoefu, uadilifu na rekodi nzuri waliyonayo katika utumishi wa umma.
Aidha, amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi kuimarisha amani, utulivu na mshikamano wa taifa pamoja na kulinda misingi ya haki, utawala wa sheria na imani ya wananchi kwa serikali.
Alisema wizara hiyo ina jukumu nyeti la kusimamia usalama wa raia na mali zao.
Rais Samia amesema uteuzi wa Profesa Palamagamba Kabudi katika nafasi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu (Kazi Maalumu) umetokana na uzoefu wake mpana, ukomavu wa kiuongozi na uelewa wa kina wa masuala ya taifa, akibainisha dhamana hiyo inalenga kuimarisha ushauri na majukumu ya kimkakati ya serikali.
Rais Samia pia ameeleza uteuzi wa Dk Richard Muyungi katika nafasi ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) unalenga kuimarisha uratibu wa sera za nchi katika kukabiliana na changamoto katika ajenda ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mabalozi wapya, Rais Samia amewataka kutambua dhamana waliyonayo ya kuiwakilisha na kulinda heshima ya Tanzania kimataifa katika nchi watakazopangiwa, sambamba na kutetea maslahi ya taifa na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia.
Aliwataka viongozi walioapa kufanya kazi kwa bidii, weledi na uzalendo akiwakumbusha kuwa wamebeba matarajio makubwa ya Watanzania.
