
“Kwa takribani wiki tatu, maandamano ya wananchi katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yamebadilika kwa kasi na kuwa machafuko ya kitaifa, na kusababisha kupotea kwa maisha ya watu wengi,” amesema Bi. Pobee, kutoka Idara ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Masuala ya Kisiasa, akihutubia kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.
Ameeleza kuwa tarehe 28 Desemba, kundi la wafanyabiashara katika Soko Kuu la Tehran lilikusanyika kupinga kuporomoka kwa kasi kwa thamani ya sarafu na kupanda kwa bei za bidhaa, hali iliyochochewa na mdororo mkubwa wa uchumi na kuzorota kwa hali ya maisha ya wananchi.
Ingawa mwanzoni maandamano hayo yalikuwa ya amani, amesema kuwa jioni ya tarehe 8 Januari, maandamano yalisambaa kote Tehran na katika miji mingine mikubwa.
Katika kujibu hali hiyo, mamlaka za Iran ziliweka zuio karibu kamili la mawasiliano, ambalo kwa kiasi kikubwa bado linaendelea hadi leo.
“Hali nchini Iran inabadilika na inatia wasiwasi mkubwa,” amesisitiza huku akirejelea kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ya kutaka pande zote kujizuia ili kuepusha madhara zaidi wakati huu ambapo makumi ya maelfu ya watu wameripotiwa kuuawa.
Niko hapa kupaza sauti za wairan ambao haki zao zinasiginwa
Katika mkutano huo, Masih Alinejad, mwandishi wa habari na mpinzani wa kisiasa kutoka Iran, amewaambia mabalozi kwamba “kile kinachohitajika sasa ili kuleta haki kwa wale wanaoagiza mauaji ya halaiki nchini Iran ni hatua za kweli na za vitendo.”
“Wairani wasio na hatia, wasio na silaha, mamilioni yao, wamezimishwa kupitia risasi, kukamatwa kwa wingi, kufungwa gerezani na kuzimwa kabisa kwa mawasiliano — hakuna intaneti, hakuna simu za mkononi wala simu za mezani. Iran iko gizani kabisa,” anasema.
Akizungumza kwa hisia huku machozi yakimtoka, Bi. Alinejad amesema “niko hapa kuleta sauti zao ndani ya chumba hiki,” anaongeza. “Niko hapa kuwaambia kwamba mauaji ya kikatili yametokea katika nchi yangu ninayoipenda, Iran.”
Tuliteswa kwa sababu ya kudai haki zetu – Mwanaharakati wa Iran
Ahmad Batebi, mwandishi wa habari mwenye uraia wa Iran na Marekani na mwanaharakati wa haki za binadamu, amewajulisha mabalozi kwamba alipokuwa mwanafunzi, alikamatwa na mamlaka za Iran kwa kushiriki katika maandamano.
Anadai kuwa aliteswa na mamlaka hizo na kulazimishwa “kukiri” mbele ya kamera kwamba alikuwa jasusi kulipwa wa Marekani.
“Sikuwahi kufanya hivyo, lakini walinitesa ili nifanye hivyo. Hali ni ileile kabisa nchini Iran kwa sasa,” anasema. “Watu wengi wasio na hatia walitoka mitaani kudai haki zao, na utawala wa Iran uliwaweka mbele ya kamera ukisema kwamba wao ni mawakala wa Mossad.” Mossad ni shirika la upelelezi la Israeli.