Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewahurumia
wanadiplomasia na raia wa kigeni wanaoishi nchini humo kufuatia vikwazo vya
mtandao vilivyowekwa nchini kote wakati wa machafuko yanayohusishwa na uchaguzi
wa Oktoba.
Ni mara ya kwanza kwa Rais kutoa maoni yake hadharani
kuhusu kuzimwa kwa mtandao, ambako kulidumu kwa zaidi ya wiki moja wakati wa
machafuko hayo.
Akizungumza na mabalozi, makamishna wakuu na wawakilishi
wa mashirika ya kimataifa Alhamisi katika mji mkuu wa Dodoma, Rais Samia
alitaka kuwahakikishia wajumbe hao usalama wao, akisema serikali itaendelea
kuwa macho ili kuzuia kurudiwa kwa usumbufu huo.
Samia alisema, “Kwa washirika wetu katika jumuiya ya
wanadiplomasia na wageni wanaoishi hapa Tanzania, poleni kwa hali ya kutokuwa
na uhakika, vikwazo vya huduma na kuzimwa kwa mtandao mliokumbana nako.”
Rais Samia alikiri kuwa vurugu zilitokea siku ya uchaguzi
na baada ya uchaguzi, lakini akatetea hatua zilizochukuliwa na serikali,
akisema madhumuni ya hatua hizo ilikuwa kulinda utulivu wa kikatiba na raia.
“Ninawahakikishia kuwa tutaendelea kuwa macho ili
kuhakikisha usalama wenu na kuzuia kujirudia kwa matukio kama hayo,” Samia
alisema.
Rais Samia alishinda uchaguzi wa Oktoba kwa asilimia 98
ya kura, baada ya wagombea wakuu wa upinzani kutoshiriki katika uchaguzi huo.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema mamia ya
watu waliuawa wakati wa machafuko hayo, ingawa serikali haijatoa takwimu rasmi
za majeruhi hadi sasa.
Wakati wa hotuba ya hadhara mwezi Desemba, Samia alitetea
hatua za vikosi vya usalama wakati wa ghasia za uchaguzi kwa kusema nguvu
iliyotumika ilikuwa “muhimu” kulinda amani na kuzuia kile
alichokitaja kama mapinduzi yaliyopangwa.
Soma zaidi: