Wananchi Msata wapatiwa elimu tiba kutoka RTSWananchi Msata wapatiwa elimu tiba kutoka RTS

PWANI: ZAIDI ya wananchi 200 wa kijiji cha Kihangaiko kata ya MSATA Wilaya ya BAGAMOYO Mkoa wa Pwani wamepata elimu ya tiba,matibabu na msaada wa vyakula kutoka kwa Shule ya Mafunzo ya Awali ya kijeshi (RTS) ya Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa lengo la kuimarisha mahusiano kati ya jeshi na wananchi.

Akizungumza jana wakati wa utolewaji wa huduma Mkuu wa Shule hiyo,Brigedia Jenerali,Sijaona Myalla alisema misaada hiyo imetolewa kwa wananchi hao kama sehemu ya zoezi la Medani la “EXERCISE MALIZA” linalofanywa na Kruta katika eneo la Msata.

Alisema kila zoezi la Kruti linalofanyika porini wamekuwa wakijenga ushirikiano na wananchi kwa kutoa huduma za afya bila malipo kwa wazee na watoto wenye changamoto mbalimbali za kiafya pamoja na kutoa chakula kwa wakazi wa eneo hilo.

“Pia tunawapatia elimu ya masuala mbalimbali ikiwemo kuhusu usalama wa maeneo yetu kwa sababu yapo yanayotumika kufanya mazoezi kuna mabomu na vitu hatari ambayo watu wanaweza kuokota wakizani kwamba ni vyuma chakavu,”alisema Brigedia Jenerali Myalla.

Pia Brigedia Jenerali Myalla alisisitiza kuwa JWTZ litaendelea kushirikiana na jamii inayowazunguka kwa kutoa huduma na misaada ya kibinadamu pale litakapohitajika kufanya hivyo ili kudumisha uhusiano mzuri uliopo

Alieleza kuwa elimu hiyo inatarajiwa kuwa endelevu ili kuongeza uelewa na ushirikiano kati yao na jamii.

Mganga Mkuu wa RTS,Meja Edwini Mboya alisema walianza kuwapatia wananchi hao huduma ya elimu kuhusu magonjwa ya kuambukizwa,usafi wa mazingira pamoja na elimu ya jumla ya afya bora.

“Tumewafanyia matibabu na upimaji wa presha, shinikizo la damu,malaria na uchunguzi qa magonjwa ya watoto ikiwemo kuhara na kifua yote hayo pia ni kwa ajili ya kuokoa afya zao,” alisema Meja Mboya.

Mwenyekiti wa mtaa wa Kihangaiko,Shabani Mkomo alisema tukio hilo limeleta tija baina ya wananchi na jeshi lao kwa kuongeza mshikamano,upendo na faraja.

Aidha wananchi wa kijiji hicho walilishukuru jeshi la wananchi kwa kuwajali jambo lililodhihirisha kwamba jeshi hilo lipo kwa ajili ya wananchi.

Mkazi wa mtaa huo,Stelah Losai alilishukuru jeshi kwa kujali afya zao kwa kuwapatia huduma ya upimaji na matibabu bila malipo.

Aidha mkazi wa mtaa huo,Kibwana Mtiko alilishukuru keshi kwa kuwapatia elimu ya afya,utunzaji wa mazingira pamoja na msaada kwa chakula na kuongeza kuwa kitendo hicho kimeongeza imani kwa wananchi dhini ya jeshi lao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *